MOSHI-KILIMANJARO.
Kamati
ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro (RCC) imeazimia kutoligawa Jimbo la Moshi
Vijijini kutokana na kutokukidhi vigezo vilivyowekwa na Tume huru ya Taifa ya
Uchaguzi (INEC)
Hayo yamejiri kwenye kikao cha dharura cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC)
kilichoketi Machi 28 mwaka huu kwa ajili ya kujadili pendekezo la ugawaji wa
Jimbo hilo.
Kikao hicho kilifanyika ukumbi wa mikutano wa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali,
vyombo vya Usalama, viongozi wa dini, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.
Akiongoza kikao hicho Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye
ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya mkoa (RCC) Nurdin Babu, alisema jimbo
hilo limeshindwa kugawanyika kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa na INEC.
Akiwasilisha taarifa ya mapendekezo ya kuligawa
Jimbo hilo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Moshi Shadrack Mhagama, alisema
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Moshi, walipendekeza Jimbo hilo ligawanywe
na kuwa Majimbo mawili ya uchaguzi, Jimbo la Mawenzi na Jimbo la Moshi Vijijini.
Alitaja moja wapo ya sababu zilizopelekea uamuzi huo ni pamoja na kigezo cha idadi ya watu, ambapo kwa majimbo ya mjini ni kuanzia wastani wa watu 600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia wastani wa watu 400,000.
Hata hivyo baada ya majadiliano ya muda mrefu kikao hicho kiliazimia kutokuligawa jimbo hilo kutokana na kutokuweko vigezo vya kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za Inec.
Akitoa mchango wake kwenye kikao hicho kuhusiana na swala hilo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi alisema kuligawa jimbo hilo kutazaa utabaka jambo ambalo si utamaduni wa Mtanzania.
“Kwa mujibu wa mapendekezo ya kuligawa jimbo haujazingatia maslahi ya watu wa tambarare ambao kimaendeleo wako nyuma ikilinganishwa na wenzao wa ukanda wa juu milimani”, alisema.
Akifafanua, Prof Ndakidemi alisema kuwa ukanda wa milimani kuna maendeleo ya kila aina zikiwemo barabara za lami, kilimo cha uhakika ambacho alisema mbali na chakula pia kinawapa wananchi wa maeneo hayo mapato.
“Ukanda
wa juu kuna shughuli za kitalii, ufugaji na maendeleo makubwa kwenye sekta za
afya, elimu pamoja na vyama vya ushirika ambavyo vimewasaidia watu kujijenga
kiuchumi”, alisema Prof. Ndakidemi.
Aliongeza, “Ukija ukanda wa tambarare hakuna barabara ya lami hata moja, kulikuwa hakuna huduma za afya za uhakika mpaka pale nilipoingia madarakani mwaka 2020 nikaenda Bungeni kupigania mpaka wakapata mradi wa hospitali ya wilaya”.
Alisema maeneo ya tambarare ambayo zamani yalikuwa hayana kitu sasa serikali imeanza kujenga shule za msingi na sekondari na nyumba za makazi kutokana na kuweko kwa huduma za uhakika zikiwemo za afya baada ya serikali kujenga hospitali ya wilaya katika ukanda huo.
Prof. Ndakidemi alisema kuwa si vyema kutumia maslahi ya kisiasa wakati wa kupendekeza kugawa majimbo badala yake watu wazingatie maslahi ya wananchi ambao ndiyo walengwa haswa yanapokuja maswala ya kimaendeleo.
“Mimi nimetoa mawazo yangu kwa uchungu kutokana na ukweli kuwa mimi kama mwakilishi wa wananchi wa jimbo la Moshi Vijijini nimeshatembelea kata zangu zote 16 zilizoko kwenye jimbo hili na ninajua changamoto za watu wangu”, alisema.