Wafanyabiashara Kilimanjaro waipongeza serikali kwa kuboresha mazingira ya ulipaji kodi

MOSHI-KILIMANJARO.

Wafanyabiashara mkoa wa Kilimanjaro wamemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya ulipaji kodi nchini.

Shukrani hizo walizitoa Februari 19,2025 mkoani hapa, wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo kwa Walipa kodi bora mkoani Kilimanjaro kwa mwaka 2023/24, hafla iliyofanyika mjini Moshi, mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea Tuzo hiyo kutoka TRA Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya (Kifaru Oil Investment Ltd) kutoka Wilayani Mwanga Suleiman Mfinanga ameipongeza TRA kwa kuanzisha Tuzo ya walipa kodi bora ambayo alisema imechangia wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari.

“Tunaishukuru sana serikali kwa kutuwekea mazingira bora ya kufanya biashara, lakini pia na elimu ya mlipa kodi inayotolewa na TRA imetuwezesha sisi wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari yetu pasipo kuweko na msuguano,”alisema Mfinanga.

Alisema utaratibu ambao TRA imekuja nao wa kuwa zawadia Tuzo imewapa moyo wafanyabiashara wengi kujitokeza na kulipa kodi kwa hiari jambo ambalo litaiwezesha Serikali kutekeleza mipango yake ya kimaendeleo.

“Walipa kodi kila siku wanakuja wapya, tuwaombe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza kasi ya utoaji wa elimu ya mlipa kodi kila wakati ili wasiwe wanawapiga faini wafanyabiashara.”alisema Mfinanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Rock Blocks ya Wilayani Rombo Fabian Woiso, alisema tuzo hiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara kutokana na ukweli kuwa inawapa wafanyabiashara nafasi ya kukutana na uongozi wa Serikali na kupata elimu mpya kila mwaka  kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.

“Hatua hii itatujengea sisi wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla kuwa na moyo wa kulipa kodi jambo ambalo alisema litaongeza idadi ya walipa kodi wengi na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kupitia makusanyo ya kodi”, alisema Woiso.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava, aliwapongeza wafanyabiashara kwa kitendo hicho cha kizalendo cha kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati.

“Niwapongeze sana wafanyabiashara wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuunga mkono juhudi za serikali za awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuhimiza kila mtu anayeshtahili kulipa kodi alipe kodi stahiki lakini kwa hiari na kwa wakati.”alisema DC Mnzava.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.