MOSHI-KILIMANJARO.
Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) mkaoni Kilimanjaro imefanikiwa kukusanya jumla ya Sh Biloni 194 kati Julai, 2024 na Januari, 2025 na kuvuka lengo la makusanyo ya nusu mwaka huo wa fedha 2024-25 ya kukusanya jumla ya Sh Bilioni 149.5
Meneja wa TRA mkoani Kilimanjaro James Jilala aliyasema hayo jana, wakati wa hafla ya Tuzo kwa Walipa kodi bora mkoani humo kwa mwaka 2023/24 iliyofanyika Moshi, mkoani hapa.
“Mkoa wa Kilimanjaro tumewekewa malengo ya kukusanya jumla ya Sh Bilioni 299 kwa mwaka wa fedha 2024/25, hivyo makusanyo hayo ya Sh Bilioni 194 ni asilimia 116 ya malengo ya nusu ya kipindi cha mwaka huu wa fedha”, alisema na kuongeza hiyo ni dalili njema kuwa Mkoa pia utavuka malengo ya makusanyo ya Sh Bilioni 299 yaliyowekwa.
Alisema mafanikio hayo yametokana na kazi nzuri iliyofanywa na uongozi wa Mamlaka hiyo ikiwemo ile ya elimu kwa umma inayohusiana na umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano Makao Makuu ya TRA Richard Kayombo alisema hafla hiyo imelenga kuwakutanisha walipa kodi ambao alisema michango yao kupitia ulipaji kodi wao ina umuhimu mkubwa pale linapokuja swala la maendeleo ya nchi na watu wake.
“Wakati Mamlaka inaanzishwa makusanyo ya kodi yalikuwa yanachangia asilimia 30 ya bajeti ya Taifa lakini sasa yanachangia asilimia 70; hii ni hatua kubwa kwa Taifa letu kwani kwa sasa tunajitegemea kwa asilimia kwenye upande wa bajeti ya Taifa letu”, alisema Kayombo.
Aliendelea kusema, “Mafanikio haya ni uzalengo ambao umeonyeshwa na walipa kodi wetu hapa nchini kwa Taifa lao; kwetu sisi TRA tutaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi wakati Serikali ikiendelea kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini ili Taifa lifikie malengo ya bajeti ya Taifa kutegemea mapato yake yenyewe”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi Godfrey Mnzava, aliupongeza uongozi wa TRA kwa kuanzisha tuzo hiyo ambapo alisema itaimarisha mahusiano kati ya Serikali na walipa kodi kupitia TRA.
“Nichukue fursa hii kutoa wito kwa wafanyabiashara kujiepuesha na tabia zinazolenga kukwepa kulipa kodi ili Serikali iendelee kupata mapato yatakayoweza kuharakisha shughuli za maedneleo”, alisema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta ya Kifaru ya Wilayani Mwanga ambayo pia ilizawadiwa kwenye hafla hiyo Suleiman Mfinanga ameipongeza TRA kwa kuanzisha tuzo ya walipa kodi bora ambayo alisema imechangia wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari.
“Hafla ya tuzo hii imewapa moyo wafanyabiashara wengi kujitokeza na kulipa kodi kwa hiari jamabo ambalo litaiwezesha Serikali kutekeleza mipango yake ya kimaendeleo”, alisema Mfinanga.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Rock Blocks ya Wilayani Rombo Fabian Woiso, alisema tuzo hiyo ni muhimu kwa wafanyabiashara kutokana na ukweli kuwa inawapa wafanyabiashara nafasi ya kukutana za uongozi wa Serikali na kupata elimu mpya kila mwaka kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
“Hatua hii itatujengea sisi wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla kuwa na moyo wa kulipa kodi jambo ambalo alisema litaongeza idadi ya walipa kodi wengi na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kupitia makusanyo ya kodi”, alisema.