MOSHI-KILIMANJARO.
Kamati ya Ushauri Mkoa wa Kilimanjaro (RCC), imeipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA), kwa jitihada zake za kuwasogezea wananchi huduma ya maji katika maeneo mbalimbali mkoani hapa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa Nurdin Babu, alitoa pongezi hizo jana, wakati akifunga mkutano uliokutana kwa ajili ya kupitia makadirio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo mkoa unatarajia kutumia jumla ya Sh Bilioni 361.6.
Aidha mkuu huyo wa mkoa aliupongeza uongozi wa MUWSA kwa kuanza kutekeleza agizo la Waziri wa Maji Jumaa Aweso la kuzifungia mita za malipo kabla (Pre-Paid Meters), taasisi za serikali likiwemo Jeshi la Polisi, jambo ambalo litawapunguzia Gharama za bili ya maji tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
“Kwa taarifa nilizonazo jumla ya mita 382 za kulipia huduma kabla ya kutumia (Pre-Paid Meters) zimefungwa katika makazi ya Polisi Manispaa ya Moshi, hongereni sana MUWSA kwa kazi nzuri hiyo.”alisema RC Babu.
Akisoma taarifa ya mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) Mhandisi Kija Limbe.
Mkuu wa kitengo cha Viwango Ufuatiliaji na Tathmini (MUWSA) Grayson Saria, alisema MUWSA kwa mwaka wa fedha 2025/2026 wanatarajia kuwa na mapato ya Sh bilioni 20.0 kati ya fedha hizo Sh bilioni 18.9 zitatokana mapato ya ndani huku Sh bilioni 1.05 ni mapato kutoka Serikali Kuu.
Saria alisema kati ya fedha hizo Sh bilioni 20, Sh bilioni 14.7 ni fedha kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, Mishahara na Sh bilioni 5.9 na OC Sh milioni 8.7.
Aidha alisema Sh bilioni 5.2 zitatumika kwenye shughuli za uwekezaji ambazo ni utekelezaji wa miradi na Sh bilioni 42 ni Mapato ya ndani huku Sh bilioni 1 kutoka Wizara ya Maji.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza MUWSA kwa kutenga Sh bilioni 18.9 kwa ajili ya Mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
“MUWSA wanafanya kazi nzuri sana, nilitamani hata halmashauri zetu ziweze kupunguza utegemezi wa fedha kutoka Serikali Kuu, watumie fedha za mapato ya ndani ili kutekeleza miradi hii ya maji.”alisema RC Babu.



.jpg)

.jpg)
.jpg)
