RUWASA kutumia Sh Bl 16.2 mwaka wa fedha 2025/2026

MOSHI-KILIMANJARO.

Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Kilimanjaro, imependekeza kutumia kiasi cha Sh bilioni 16.2 kwa mwaka wa fedha 2025-2026, lengo kuu likiwa ni kuboresha huduma za maji safi na salama katika maeneo ya vijijini.

Hayo yamo kwenye taarifa ya mapendekezo ya kutumia Sh bilioni 16.2  kwa mwaka wa fedha wa 2025-2026 kwa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Kaimu Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Getruda Mushi, aliyasema hayo jana, wakati akiwasilisha taarifa ya mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2025/2026 kwa Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Mhandisi Mushi ; alieleza kuwa bajeti hiyo itasaidia kukamilisha miradi inayoendelea, ikiwemo miradi ya maji katika Wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Alisema mpango wa bajeti hiyo umelenga kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa na RUWASA kwa maeneo ya vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.

 “RUWASA inapendekeza kutumia kiasi cha Sh bilioni 16,522, 256, 89. kwa bajeti ya mwaka 2025-2026 na kwamba fedha hizi zitakwenda kutekeleza miradi ya maji inayoendelea katika maeneo ya vijijini.”alisema.

Aliitaja miradi inayoendelea kutekelezwa na RUWASa kuwa ni pamoja na miradi miwili yenye thamani ya Sh bilioni 2.3 iliyoko wilaya ya Hai, Siha miradi miwili yenye thamani ya Sh bilioni 3.3 wilaya ya Same miradi mitatu yenye thamani ya Sh bilioni 6.2, Wilaya ya Mwanga miradi mitatu yenye thamani ya Sh bilioni 1.9 na Wilaya ya Moshi vijijini miradi minne yenye thamani ya Sh bilioni 2.6

Aidha alisema kuwa kupitia bajeti hiyo pendekezwa wananchi wapatao 139,182 watafikiwa na huduma ya maji safi na salama kwenye wilaya hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, alitoa maelekezo kwa RUWASA kuhakikisha kwamba wananchi wote walioomba maji kufungiwa mita za malipo kabla (Pre-paid Meters) ili kuachana na suala la wasoma mita kugombana kila siku na wateja wao.

“Nimeelekeza watu wote wafungiwe (Pre-paid Meters) jambo ambalo litasaidia kupunguza msuguano baina ya wasoma mita na wateja, wewe unapokuwa na simu yako inapokuwa haina vocha si una kwenda kununua vocha ili uweze kuwasiliana na ndugu zako?? Lakini sisi sote tunatumia umeme wa  luku!? ….

Aidha Babu alisema kuwa “Unapoisha si tunakwenda kununua luku,  maana huwezi kukaa gizani pasipo kuwa na mwanga wa umeme na suala la maji tunataka twende huko kwa mkoa wetu wa Kilimanjaro watu wote tunataka wafungiwe mita za malipo kabla (Pre-paid Meters) ili tusiendelee kugombana na watu kila siku,”alisema Babu.

Alisema kuwa licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu maji, ukusanyaji na usambazaji wa maji, ni jukumu la kila Mtanzania sasa kutunza vyanzo vya maji.

“Tunalo jukumu kubwa la kutunza na kuhifadhi vyanzo hivi vya maji; na eneo hili tuna mgogoro mkubwa kwani vyanzo vyetu vya maji vinaharibiwa, hivyo ni wajibu wetu kuvitunza vyanzo hivi.”alisema.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.