Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA),imesema kwamba kumekuwepo na matumizi mabaya kwa baadhi ya warusha angani vifaa vya kieletroniki visivyo na rubani (drones) pasipo kupata kibali maalum kutoka kwa mamlaka hiyo na kuwaonya kuacha tabia hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Salim Msangi, aliyasema hayo Februari
17,2025 mkoani Kilimanjaro, wakati akikabidhi misaada ya vitu mbalimbali kwa
wafungwa na mahabusu walioko katika Gereza Kuu Karanga Moshi.
"Kumekuwepo na
matumizi mabaya ya drones hizo kwa baadhi ya watu mbalimbali wakiwemo waandishi
wa habari na kuwataka kufuata sheria za nchi kama zinavyo wataka kwa ajili ya
kuopata kibali cha kurusha ndege hizo."alisema.
Alisema Kanuni za
Ki-Usalama za Kudhibiti matumizi ya Ndege zisizo na Rubani za Mwaka 2018 Mamlaka
ya Anga inawakumbusha hatua za kuzingatia ili kusajili Ndege hizo.
Amesema mtu yeyote wakiwemo Wandishi wa habari anapotaka kuitumia Ndege hiyo (drones) ni lazima anatakiwa kupata kibali cha kuitumia, anapoitumia wakati hujapata kibali akikamatwa anaweza akashtakiwa.
Akizungumzia msaada huo wakati akikabidhi kwa uongozi wa Gereza la Karanga Mkurugenzi huyo, alisema ni sehemu ya kile ambacho wanakipata na kuwasaidia wenye uhitaji wakiwemo wafungwa na mahabusu walioko
magerezani na kuziomba taasisi zote za umma na binafsi, kuwasaidia wafungwa hao walioko magerezani, kwani wanahitaji huduma muhimu za kijamii.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Leornad Burushi ameushukuru uongozi Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA Tanzania kwa msaada huo na kuahidi kile kilicholetwa kitatumika kama ilivyokusudiwa na kutoa wito kwa jamii kuwa na moyo wa kusaidia wahitaji hususani waliopo gerezani.
Aidha alisema changamoto kubwa iliyoko katika Gereza hilo ni upungufu wa magodoro pamoja na mashuka na kuwaomba wadau wengine kuona umuhimu wa kuwatatulia changamoto hiyo kama ambavyo wamefanya TCAA.








