MOSHI.
Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Mkoa wa Kilimanjaro kimesema kutokana na mikakati waliyojiwekea watahakikisha wanashinda katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu kote nchini.
Mwenyekiti wa SAU Mkoani humo Isaack Kereti ameyasema hayo Februari 18,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi mkoani hapa kuhusiana na zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu, ambapo wanachama wenye sifa za kugombea wanakaribishwa ili kuja kukijenga chama hicho.
Amewataka wanachama wote wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu, ili kushirikiana kukijenga chama hicho na kukivusha katika uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais, baadae mwaka huu.
Amesema mchakato wa uchaguzi tayari umekwisha kuanza ambapo zoezi la kuchukua na kerejesha fomu lilianza februari 13 na litafikia tamati februari 22, mwaka huu.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa SAU Mkoa, Mohamed Amiri Shemvaa amesema chama hicho kina tarajia kufanya uchaguzi wa kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na kufuata kanuni na taratibu zote za uchaguzi kwa watia nia wote wa uchaguzi huo.
Amesema maandalizi hayo ni kwa ajili ya kwenda kushika dola katika uchaguzi mkuu wa nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza mkurugenzi wa uchaguzi Sau Mkoa, Ben Chuwa amesema utaratibu umepangwa kwa ajili ya kuhakikisha wale wote watakaochukua fomu kushiriki uchaguzi wamekidhi vigezo.
Hadi kufikia Februari 18, Jumla ya watu wanne tayari wamejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi mbalimbali akiwemo Isaack Kireti ambaye amechukua kuomba kutetea nafasi yake ya uenyekiti Mkoa wengine waliochukua fomu ni pamoja na Gasper Fundi (makamu mwenyekiti), Mohamed Amiri (katibu) na Richard Shangali (katibu msaidizi)