Kituo cha The Creator Share Foundation kimeiomba serikali ruzuku ya madawa kwa watoto wenye mahitaji maalumu


MOSHI.

Kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalumu cha The Creator Share Foundationi kilichopo Uchira, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi,mkoa wa Kilimanjaro kimeiomba serikali kuwapatia ruzuku ya madawa, ili kuweza kuwahudumia vyema watoto wanaowalea.

Ombi hilo linatokana na changamoto za kifedha zinazokikumba kituo hicho katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata huduma bora za kiafya.

Akizungumza wakati wa kupokea misaada ya vitu mbalimbali kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, Afisa rasilimali watu wa kituo hicho, Judith Shio alisema changamoto kubwa waliyo nayo ni ya kifedha ambapo asilimia 90 ya watoto wanaowahudumia kutumia dawa kila siku.

Alisema kituo hicho kina jumla ya watoto 171 wenye mahitaji maalumu ikiwemo wenye ulemavu wa aina mbalimbali, kimetajwa kuwa na mahitaji makubwa ya madawa kutokana na watoto wanaohudumiwa hapo kuugua mara kwa mara.

“Changamoto tuliyo nayo ni kwamba asiliamia 90 ya watoto wanatumia dawa kila siku, na dawa hizi zinauzwa kwa gharama kubwa”alisema Shio.

Aliongeza kuwa “Watoto hawa tunawahudumia kwa kuwapa msaada, lakini hatuna ruzuku katika matumizi ya dawa, tunanunua katika maduka ya kawaidi, tunaamini serikali kupitia wizara ya afya wanaweza kututambua na kutupatia punguzo kwa ajili ya dawa kwani shirika letu lipo kwa ajili ya kusaidia watoto na siyo biashara”.

Akizungumzia msaada waliopewa na TRA mbali na kushukuru wamesema itawasaidia kuwasogeza mbele kwa kuwa mahitaji waliyo nayo katika kuwahudumia watoto hao ni makubwa.

“Tunao jumla ya watoto 171 ambapo watoto 120 ni wenye changamoto ya mahitaji maalum, ambao walmezaliwa na ulemavu, hivyo msaada tulioletewa umekuja wakati muafaka”.

Ameongeza kuwa“Tunaishukuru TRA kwa kuonesha kututambua wameona juhudi zetu katika kuwahudumia hawa watoto na kuguswa kuja kutoa misaada hii”.

Akizungumza baada ya kukabidhi misaada hiyo, Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro James Jilala amesema wamepeleka misaada hiyo kama sehemu ya shukrani kwa mlipa kodi.

“Hii ni wiki ya shukrani kwa mlipa kodi, sisi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)tuliona ni muhimu kuja kujumuika na kituo hiki kuwatembelea watoto hawa na kuwapatia misaada ya kibinadamu”alisema Jilala

Aliongeza kuwa “Hawa wanamahitaji makubwa sana, tunamshukuru kiongozi wa hapa kwa Baraka alizojaliwa na Mwenyezi Mungu na kuanzisha kituo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum”.

Alitoa wito kwa jamii kujenga utamaduni wa kuwatembelea watoto wenye mahitaji maalumu na kuwasaidia ili kutimiza mahitaji yao ya msingi.






Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.