MOSHI.
Halmashauri ya
Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, imetenga jumla ya Sh bilioni 1 kwa ajili
ya maboresho ya uwanja wa michezo wa Majengo.
Lengo kuu la mpango
huo ni kutumia fursa ambazo zitatokana na Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa
michuano ya AFCON mwaka wa 2027.
Hayo yameelezwa na
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mwl. Mwajuma Nasombe, wakati wa kikao cha Baraza
cha bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 kilichofanyika,
mwishoni mwa wiki.
“Fedha hizi ni ziada
ya Sh milioni 600 ambazo tayari zilishatumika katika ujenzi wa uwanja huo ambao
umechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa michezo haswa mpira wa miguu Manispaa ya
Moshi na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla”, alisema.
Mwl. Nasombe alisema
mbali na fursa hiyo pia uamuzi huo umelenga kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu
Hassan zinazolenga kuiinua sekta ya michezo hapa nchini ambayo pia imepelekea
Tanzania kuandaa michuano ya AFCON kwa Ushirikiano na Mataifa mengine ya Afrika
Mashariki ya Kenya na Uganda.
“Fursa ambayo tunataka
kuichangamkia kupitia uwekezaji wa uwanja wetu wa Majengo ni ile ya timu ambazo
zitashiriki michuano ya AFCON mwaka 2027 kwenye kituo cha Arusha
wauutumie na uwanja wetu wa Majengo kwa ajili ya mazoezi yao”, alisema.
“Timu zitakazoshiriki
michuano hiyo zitahitaji viwanja vya kufanyia mazoezi hivyo uwanja wa Majengo
utakuwa na fursa ya kupata walau timu moja ambayo itautumia na hivyo kuongeza
mapato ya hamashauri yetu”, alisema.
Aidha mkurugenzi huyo
alitoa wito kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro na wale wa Mikoa ya
jirani kujitokeza kuunga mkono juhudi za halmashauri hiyo katika maboresho ya
uwanja huo ili nao wanaufaike kupitia fursa hiyo ikiwemo kujitangaza kupitia
uwanja huo.
Alisema “Fursa hii ni
muhimu ambayo inaweza kuchangia biashara zao haswa ikitiliwa maanani ya kuwa
mchezo wa mpira wa miguu ni maarufu na matangazo yake hufika mbali kupitia
michuano mbalimbali ya soka ya ndani na yale ya Kimataifa”, alisema.
Kwa upande wake Meya
wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo alisema kuwa gharama
za ukarabati wa uwanja huo unatokana na makusanyo ya Sh bilioni 10 ambayo
yatakuwa ni mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2025/26.
“Maboregso ya uwanja
huu yatahusu pamoja na mambo mengine uwekaji wa viti vya watazamaji, ufungaji
wa taa za uwanjani, nyasi bandia pamoja na miundombinu ya kuingia na kutoka
uwanjani”, alisema Mhandisi Kidumo.
Nao baadhi ya wadau wa
michezo Manispaa ya Moshi, wameupongeza uongozi wa Manispaa hiyo kwa
uamuzi huo ambao walisema utaendelea kuitangaza halmashauri hiyo Moshi
kupitia sekta ya michezo.
“Uweko wa uwanja huu
ni hatua kubwa ya kimaendeleo kutokana na ukweli kuwa Manispaa ya Moshi
haikua na uwanja na badala yake walikuwa wanalazimika kutumia viwanja vya
taasisi mbalimbali pale mahitaji yanapotokea”, alisema Abdalla Mtwenge mdau wa
michezo Moshi Mjini.
Mtwenge alisema mbali
na kutumika kwa ajili ya michezo aina mbalimbali uwanja huo pia utatoa fursa ya
wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wale wa vyakula na usafirishaji kuongeza
mapato yao wakati wa mashindano mbalimbali yakayofanyika uwanjani hapo.
Kwa upande wake mdau mwingine wa michezo Wilson Enock alisema uamuzi wa Manispaa ya Moshi kuuboresha uwanja huo kutaongeza mapato ya halmshauri na fursa kwa wenyeji kuboresha hali zao za kiuchumi.



