MOSHI-KILIMANJARO
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, kimemfukuza uanachama kada wa chama hicho Mchungaji Dk. Godfrey Malisa kwa kosa la kukosa maadili ikiwemo kupinga maamuzi ya Mkutano Mkuu wa CCM wa kumteua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Katibu wa CCM mkoa wa kilimanjaro Mercy Mollel amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na Malisa kukiuka taratibu za chama hicho kila mara kwa kupinga maazimio ya Mkutano mkuu wa kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea wa urais.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizikia kwa Kikao cha Halmashauri Kuu ya chama Mkoa, Mollel alisema Mchungaji Malisa amefukuzwa uanachama kuanzia Februari 10,mwaka 2025.
"Leo tulikuwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro, ambacho pamoja na mambo mengine kimemfukuza Dk. Godfrey Malisa aliyekuwa mwanachama wa CCM kwa kosa la kukosa maadili."alisema Mollel.
Mollel amesema hatua ya kufukuzwa kwa kada huyo inatokana na kauli zake ambazo amekuwa akizitoa, kutia vyombo mbalimbali vya habari za kupinga maamuzi ya Mkutano mkuu wa chama hicho Taifa uliofanyika Januari 19,2025 akidai kuwa maamuzi ya kupitisha mgombea Urais wa chama hicho ulikiuka Katiba ya chama hicho Tawala.
Itakumbukwa kuwa Januari 27 mwaka huu, kada huyo aliitisha vyombo vya habari mkoani hapa na kutoa kauli za matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na kwenye nchi yetu.
"Malisa amekuwa akisema maamuzi ya mkutano mkuu yamevunja Katiba ya CCM. Kwa mujibu wa kanuni za maadili ya chama chetu kifungu cha 6 kifungu kidogo cha tatu kinaekeza waziwazi, hivyo amekosa sifa za kuwa mwanachama."alisema.
Januari 19, 2025 Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulimteua rasmi Mwenyekiti na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea wa urais kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Uamuzi huo wa kihistoria ulionyesha imani kubwa na matumaini makubwa ambayo CCM inayo kwa uongozi thabiti na wa kimkakati wa Rais Samia, pamoja na dhamira yake isiyotetereka ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
Katika kipindi chake cha uongozi, Tanzania imeshuhudia mafanikio makubwa katika ukuaji wa Uchumi, Ujenzi wa Miundombinu, Maboresho ya Huduma za afya, na kukuza Demokrasia kupitia Falsafa yake ya “4Rs.”


