HAI.
Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA), imetoa maelekezo kwa Mameneja wa RUWASA kote nchini, kuhakikisha agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kufunga mita za malipo ya kabla kwa wateja (PRE-PAID METERS), linazingatiwa kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi wote.
Mwenyekiti wa Bodi ya RUWASA Makao Makuu Jijini Dodoma Mhandisi Ngwisa Mpembe, ametoa maelekezo hayo Februari 10, 2025 wakati wa ziara ya Wajumbe wa Bodi na Wataalam wa RUWASA, walipotembelea na kukagua miradi ya maji Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Mhandisi Mpembe alisema kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa agizo hilo la Rais Samia, RUWASA hawana budi kuhakikisha utekelezaji wa agizo hilo unafanyika vizuri ili kila mwananchi anakuwa na mita hiyo.
Akiongea na wakazi wa kitongoji cha Kimaroroni, kijiji cha
Matowo Kata ya Masame Kusini Wilayani humo wakati wa uzinduzi wa kilula cha
maji Mpembe alitoa wito kwa wakazi hao kuhakikisha wanailinda miundombinu ya
mradi huo ili uwe endelevu kwa manufaa ya wakazi wa sasa na wale wa kizazi
kijacho.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Mhandisi Wolta Kirita, alisema ziara hiyo ililenga kukagua, kuangalia skimu za maji namna zinavyotunzwa, kufunga mita za malipo ya kabla kwa wateja, sambamba na kuangalia miradi inayotekelezwa na RUWASA mkoani humo.
“Naipongeza Bodi ya Maji Uroki-Bomangombe kwa kutimiza wajibu wake wa kutumia fedha ambazo wanazikusanywa kwa ajili ya kufanya matengenezo na kuwajengea kilula cha maji wakazi wa Kimaroroni ili kuwasogezea karibu wananchi huduma ya maji karibu na maeneo yao.”alisema Mhandisi Kirita.
Alisema mafanikio ya upatikanaji maji katika kitongoji cha Kimaroroni yamepatikana kutokana na mradi wa Kikafu-Bomang’ombe ambapo chanzo kilichotumika ni cha Kikafu Soka kilicho hapa wilayani Hai.
Aidha alisema RUWASA ina jumla ya vyombo vya watumia maji 992 na
kati ya hivyo vyombo 979 vimeshaingizwa kwenye mfumo wa ukusanyaji wa mauzo ya
maji ambavyo vinatoa bili kwa kutumia contro number jambo ambalo
imesaidia ukusanyaji wa maduhuli kuongezeka.
Akisoma taarifa ya miradi ya maji Meneja wa RUWASA Wilaya ya Hai Mhandisi Emmanuel Mwampashi alisema kuwa mradi huo wa Kikafu-Bomang’ombe umeanza kutekelezwa Disemba, 2021 na kukamilika Febuari, 2024.
Alisema mradi huo ulitekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Maji wa Taifa NWF kwa gharama ya Sh bl 2.8 na kuzinduliwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango Machi 20, 2024.
Mhandisi Mwampashi alisema kuwa RUWASA imebuni mrdai mwingine wa Kikafu-Kwasadala wenye thamani ya Sh milioni 997ambao unatarajiwa kuwahudumia wakazi wa kitongoji cha Matowo na kijiji cha Kwasadala, Wilayani Hai.
Awali akizungumza Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Weransari Munisi alisema kuwa kukamilika kwa mradi wa Kikafu-Bomang’ombe kumechangia kuongezeka kwa watu katika mji wa Bomang’ombe jamabo ambalo limepelekea kuongezeka kwa shughuli za kimaendeleo na hivyo kuimarisha uchumi wa wilaya ya Hai.









