Mbunge Pricus Tarimo Akabidhi Gari la Wagonjwa Jimboni Moshi

MOSHI.

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Huduma ya Lishe imetoa magari matano ya dharura (Ambulance) kwa lengo la kubebea wagonjwa sambamba na na kujenga vituo vitatu vya afya katika kipindi cha miaka mitatu, katika Jimbo la Moshi Mjini Mkoani Kilimanjaro

Mbunge wa Jimbo la Moshi mjini Priscus Tarimo, aliyasema hayo jana wakati wa hafla fupi ya kukabidhi garo moja la wagonjwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi.

Tarimo alisema serikali imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya, jambo ambalo limewezesha Jimbo la Moshi Mjini kupata magari ya kubebea wagonjwa matano na kujengwa vituo vya afya vitano kutoka viwili vilivyokuwepo hapo awali.

“Uwekezaji ambao umewekwa katika sekta ya afya umenza kuzaa matunda na kwenye hili nichukue fursa hii kwa dhati kabisa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya” alisema Tarimo.

Aliongeza “Kutokana na uwepo wa gari hili la wagonjwa  hatutarajii mama mjamzito awe na changamoto ya kufika hospitali kwa ajili ya kujifungua halafu  gari liwe kwenye shughuli zingine, gari hili limeletwa kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wote bila ubaguzi lengo ni kuwafikia watu wasiokuwa na uwezo,”alisema.

Aidha Mbunge Tarimo, aliwaomba Watumishi na Wataalamu kwa ujumla kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni ili wananchi waweze kufurahia nchi yao pamoja na huduma zinazotolewa na serikali.

"Nimetoka kukabidhi gari jingine jipya la kubeba wagonjwa na kufikisha idadi ya magari ya wagonjwa tuliyoyapata kwa awamu hii yafikie matano, hapa kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa Mawenzi gari hili ni la pili kwa awamu hii lakini Moshi Manispaa wamepata gari mbili na KCMC moja"alisema Mbunge Tarimo.

Alifafanua kuwa kwa hospitali ya rufaa ya mkoa Mawenzi yako maendeleo makubwa kuanzia jengo la Mama na mtoto kukamilishwa, kuwepo kwa CT Scan, ICU Mpya, jengo la dharura, jengo la upasuaji la kina baba lakini pia tuna fedha za jengo la upasuaji na hata kitengo cha kusafisha damu".

Akizungumzia ujenzi wa vituo vya afya Tarimo alisema, serikali inajenga hospitali ya Wilaya ujenzi, lakini pia imetoa fedha za kujenga vituo vya afya viwili ambavyo tayari vimekwisha kukamilika, ambapo kituo kimoja kipo kata ya Shirimatunda ambacho kimekamilika na kingine kipo kata ya Msaranga- maeneo ya Msandaka ambacho kinaelekea kumamilika.

“Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 tutapata Sh milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kwenye zahanati ya Kiborlon na hivyo kufikisha vituo vitano."

Alisema wakati serikali inaendelea kufanya huo uwekezaji mkubwa kwenye afya pia inaangalia namna huduma hizo zitakwenda kuwa stahimilivu na kuhakikisha vifaa tiba na dawa zinapatikana ili wananchi wote waweze kuoata huduma bora.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya ushauri Hospitali ya rufaa Mawenzi, Mchungaji Emmanuel Maro, aliishukuru serikali kwa jitihada inayofanya za kuhakikisha wananchi wanapata hufuma bora za afya.

"Kwenye hospitali yetu  leo tena tumepokea gari la kubebea wagonjwa, hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ta awamu ya sita chini ya Rais Samia, katika kuzisaidia hospitali za mikoani ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi ambao ni maskini kwa kuwafikishia huduma za afya na kuwawezesha kuzifikia kwa urahisi zaidi"alisema Maro.

"Kwa niaba ya bodi na menejiment ya hospitali tunaiunga mkono serikali na tunafanya kazi kubwa kuwasaidia watanzania wenzetu wapate matibabu na huduma bora za viwango vya juu kabisa."

Naye Mganga mfawidhi wa Mawenzi, Dk. Edna-Joy Munisi alisema gari hiyo ni ya pili hospitali hapo kukabidhiwa na kuishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kuwa mgonjwa anapohitajika kusafirishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine itakuwa rahisi.

"Hospitali yetu ya Mawenzi imepata magari mawili ya wagonjwa mapya, tunaishukuru sana serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini, kwani kabla ya hapo tulikuwa na gari moja na sasa tumepokea gari jingine na hivyo kufuikisha gari ya pili hivyo hii inamaanisha kwamba hakutakuwa na mkwamo wowote wa usafirishaji wa wagonjwa kutoka hapa kwenda rufaa Kanda au vituo vingine vinapopata changamoto inakuwa rahisi kuchukua gari".









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.