Manispaa ya Moshi kutekeleza miradi mitatu ya Kimkakati mwaka wa fedha 2025/2026


MOSHI.

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, imejipanga kutekeleza miradi mitatu ya kimkakati kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kupitia mapato yake ya ndani.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Mwl. Mwajuma Nasombe, aliyasema hayo Februari 7,2025 wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi kwa ajili ya kupitisha rasimu ya makadirio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Nasombe aliitaja miradi ya kimkakati ambayo watakwenda kuitekeleza ni pamoja na ujenzi wa vibanda vya biashara kuzunguka soko la mbuyuni, ujenzi wa vibanda vya ghorofa katika viwanja vya Uhuru Park, ujenzi wa ukumbi wa sherehe kata ya Kilimanjaro, sambamba uwanja wa michezo wa majengo ambao watakwenda kuuboresha kwa viwango vya kimataifa ili uweze kutumika  kwa ajili ya michuano ya michuano ya AFCON itakayofanyika mwaka 2027.

"Tunavyo vipaumbele vitatu  kwa mwaka 2025/2026, vipaumbele hivi ni pamoja na umaliziaji wa miradi vipolo, ukusanyaji wa mapato pamoja na ujenzi wa miradi mipya ambayo itapelekea kutuongezea mapato,"alisema  Mwl. Nasombe.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Baraza hilo limepitisha bajeti ya Sh bilioni 53.2 ambapo mapato ya ndani Sh bilioni 9.9, matumizi mengine Sh bilioni 1.2, Mishahara Sh bilioni 32.1na miradi ya maendeleo Sh bilioni 9.8.

Akizungumza Meya wa Manisoaa hiyo, Mhandisi Zuberi Kidumo amesema  Halmashauri hiyo imepitisha mapendekezo ya bajeti ya Sh bilioni 53.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, huku makusanyo ya ndani yakitarajiwa kufikia Sh bilioni 9.9.

 “Wakati Rais Samia Suluhu Hassan, anaingia madarakani mwaka 2021 bajeti ya Manispaa ilikuwa Sh bilioni 41.7  na kwa kipindi cha miaka minne ya Rais Samia imeongezeka na kufikia Sh bilioni 53.2 ambapo mapato ya ndani, mwaka 2021 yalikuwa Sh bilioni 6.1 na leo tumepitisha Sh bilioni 9.9 ongezeko la takribani Sh bilioni 3.7 haya ni mageuzi makubwa.”alisema Kidumo.

Kwa upande wake Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo, aliupongeza  uongozi wa Halmashauri  hiyo kwa jitihada inazochukua katika kuongeza ukusanyaji wa mapato, huku  akitoa wito kwa nadiwani kuonyesha ushirikiano ili kuongeza nguvu ya ukusanyaji.

"Nikupongeze Mkurugenzi  Mwajuma Nasombe na timu yako ya wataalam, lakini pia Mstahiki Meya Zuberi Kidumo na Baraza lako la Madiwani kwa hatua kubwa tuliyopiga ya ukusanyaji mapato na mwaka huu wa fedha naona tutavuka malengo ya ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani na hivyo kufikia Sh bilioni, 10 kwani mpaka sasa tumefikia asilimia 63.”alisema Mbunge Tarimo.Naye Diwani wa kata ya Kiboriloni Frank Kagoma alipongeza utendaji kazi wa mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mwajuma Nasombe, uliowezesha kupandisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kuongezeka kutoka Sh bilioni 6.1 mwaka 2021 hadi kufikia Sh bilioni 9.9.

"Nimeona kazi kubwa inayofanywa na mkurugenzi wa Halmashauri hii, amekuwa mwema na ameonyesha ushirikiano bila ubaguzi, kwani mwaka jana mwezi kama huu tulikuwa tunaongelea asilimia 32 ya makusanyo lakini leo tunaongelea asilimia 63, hakika zipo jitihada zimefanyika, tunapaswa kukupongeza wewe na watendaji wako"alisema Kagoma.

Awali  akizungumza Mwenyekiti wa Chama cha Mapunduzi (CCM) Moshi Mjini, Faraji Swai na Katibu Frida Kaaya  kwa pamoja waliupongeza uongozi wa halmashauri hiyo chini ya mkurugenzi wake Mwajuma Nasombe na Baraza la Madiwani, huku wakitoa wito  kwa watendaji kutumia lugha nzuri na yenye staha wakati wa ukusanyaji kodi.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.