MOSHI-KILIMANJARO
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ya Manispaa ya Moshi imemshukuru Mstahiki Meya wa Jiji la Marburg nchini Ujerumani Dk. Thomas Spies, kwa msaada wake ambao wameipatia Manispaa hiyo gari la zimamoto na uokoaji waliloomba kusaidiwa kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya moto.
Shukrani hizo zimetolewa jana na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo, wakati akipokea gari la zimamoto na uokoaji ambalo wameletewa kutoka Jiji la Marburg nchini Ujerumani
“Kama mtakumbuka Oktoba 25, 2023, marafiki zetu kutoka Ujerumani walitutembelea hapa Moshi, tuliwaeleza changamoto zetu zinazotukabiliana ikiwemo uhaba wa gari la zimamoto, wenzetu hawa walituahidi wakirudi Ujerumani watatusaidia kutupatia magari mawili ya zimamoto, kile walichotuahidi wameanza kukitekeleza kama ambavyo tulikubaliana,”alisema.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kidumo, alisema ushirikiano wa Miji hii miwili inahusisha ushirikiano katika sekta za Majanga na Zimamoto.
“Marburg ni Jiji ambalo limejikita kwenye masuala ya elimu zaidi hususani ile inayohusiana na afya, tiba na kinga, ushirikiano huu utakuwa ni muhimu sana katika kuboresha sekta ya afya katika Manispaa yetu”, alisema Mhandisi Kidumo.
Aidha alisema Jiji la Marburg pia limebobea katika kupambana na Majanga eneo la uokoaji hasa Zimamoto hivyo uhusiano huo utasaidia kupata vifaa vya zimamoto pamoja na elimu juu ya uokoaji na kupamabana na majanga kama vile mafuriko na matetemeko ya ardhi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Moshi Priscus Tarimo,aliwashukuru Manispaa ya Moshi kwa kuendelea kujenga mahusiano hayo mazuri ya ushirikiano kwani yana manufaa makubwa kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi na mji dada wa Marburg.
“Tunawashukuru sana wadau wetu Marburg. haya ni matokeo ya hoja binafsi ya kushawishi halmashauri ziweze kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na uokoaji katika kuwahudumia wananchi”alisema Mbunge Tarimo.
Awali akizungumza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe, alisema wanalazimika kuomba kupatiwa gari la zimampoto, baada ya Manispaa ya Moshi kuwa na majanga mengi ya moto, kutokana na zimamoto mkoa kuwa na uhaba wa magari ya ukoaji.
Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Kilimanjaro Mrakibu msaidizi Jeremiah Mkomagi,aliushukuru uongozi wa Manispaa ya Moshi kwa namna ambavyo wamekuwa na ushirikiano wa Mji dada na Jiji la Marburg.

















