MBOKOMU-MOSHI
Serikali ya awamu ya sita
imeendelea na maboresho makubwa ya miundombinu ya kutolea huduma za afya ikiwa
ni pamoja na ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na ukamilishaji wa ujenzi wa
hospitali mpya za mikoa hapa nchini.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa
ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Kilimanjaro Best
Simba, aliyasema hayo Februari 3,2025 wakati wa ziara yake Kata za Old Moshi
Mashariki, Mbokomu, Uru Kusini na Kirua Vunjo zilizoko Jimbo la Moshi Vijijini
mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na Wananchi Kata
ya Mbokomu, ikiwa ni kuadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi
CCM, alisema mafanikio yaliyopatikana nchini, katika kipindi cha miaka 48
hayakuja kwa bahati mbaya, bali yalitafutwa kwa juhudi na mikakati thabiti.
Alisema kwenye sekta ya
afya; Simba alisema serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya kutolea
huduma za afya ngazi ya msingi zimejengwa, ikiwemo ukarabati wa hospitali kongwe.
Alisema pia serikali
imeimarisha huduma za uchunguzi wa mionzi kwa wagonjwa, ununuzi wa vifaa tiba
vya uchunguzi ambavyo vinapatikana kuanzia ngazi ya tospitali ya taifa hadi hospitali
za Rufaa za Mikoa (RRHs) na Halmashauri.
“Kupitia mafanikio haya CCM imekuwa mstari wa mbele ndani ya miaka 48 kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yanaonekana wazi katika nchi nzima chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,”alisema Simba.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini Ramadhan Mahanyu, aliendelea kuwahimiza wananchi kuendelea kuiamini serikali kwani katika wilaya hiyo Sh bilioni 90 zimetumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Wilaya ya Moshi Vijijini tuna majimbo mawili, jimbo la Vunjo limepata Sh bilioni 45 na jimbo la Moshi vijijini pia limepata bilioni 45 na hivyo kuleta jumla ya Sh bilioni 90,ambazo zimewezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo,”alisema Mahanyu.


