Waziri wa Afya Jenista Mhagama (kulia), akimpongeza Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH), Dkt. Leonard Subi, kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ya kimkakati iliyowezesha kuboresha sekta ya afya hospitalini hapo.
KIBONG’OTO-SIHA.
Serikali imesema inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mkurugenzi
wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH), Dkt.
Leonard Subi na menejimenti yake jambo ambalo limewezesha kuboresha
sekta ya afya hospitalini hapo na hivyo kuipa heshima nchi ya Tanzania kwenye
tasnia ya afya ulimwenguni kote.
Waziri wa Afya Jenista Mhagama, alitoa pongezi hizo Januari
10,2025, wakati akizindua Bodi mpya ya uongozi ya hospitali hiyo, hafla
iliyofanyika hospitalini hapo.
Alisema hospitali ya Kibong’oto, imetoa mchango mkubwa kupitia
tafiti zake mbalimbali ambazo zimechangia pamoja na mengine kupunguza muda wa
matibabu kwa wagonjwa wa Kifua Kikuu, kutoka miaka miwili hadi kufikia miezi 9
lakini pia wameweza kupunguza matumizi ya dawa nyingi kwa muda mrefu katika
kutibu ugonjwa huo.
“KIDH imetoa mchango mkubwa uliopelekea kuondolewa kwa tiba ya
Kifua Kikuu kwa kutumia sindano; mafanikio haya yamelipatia Taifa heshima kubwa
Kimataifa”alisema.
Alisema kuwa matumizi ya sindano kwa muda mrefu na hata yale ya
dawa, yalikuwa yakipelekea wagonja wengi kushindwa kumalizia muda wa matibabu
waliyowekewa na hivyo kusababisha ugonjwa huo kufikia hali ya usugu, hali
ambayo ilimfanya mgonjwa wa Kifua Kikuu kuwa na hali mbaya zaidi.
Waziri Mhagama, alisema kuwa kwa kipindi cha miaka
mitatu ambayo Dk. Subi amekuwepo katika hospitali hiyo, yako mageuzi makubwa
aliyoyafanya, ikiwemo usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maendeleo
inayotekelezwa ndani ya hospitali hiyo.
“Ndugu zangu mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, kwa
kipindi cha miaka mitatu sisi serikali, tumeshuhuduia mageuzi
makubwa ya kimaendeleo na kimkakati yanayofanyika kwenye hospitali hii,
imedhihirisha ni aina gani ya kiongozi tuliyenaye anayesimamia hospitali hii,
lakini pia na aina ya watumishi ambao wanafanya kazi katika hospitali ya
Kibong’oto,”alisema Waziri Mhagama.
Akizungumzia Bodi hiyo mpya, Waziri Mhagawa alitoa rai kwa uongozi
huo kuendelea kushirikiana na menejimenti ya hospitali hiyo ili kuendeleza
mafaniko ambayo yamepatikana.
Akiwasilisha taarifa ya hospitali hiyo, Mkurugenzi wa KIDH Dk.
Leonard Subi, alisema kuwa mafanikio yaliyopatikana hospitalini hapo yametokana
na tafiti mbalimbali zinazofanwa na wataalam walioko hospitalini hapo.
“Tunaishukuru Serikali kwa mchango wake mkubwa kwa hospitali yetu
hii, zikiwemo fedha zaidi ya Sh bilioni 22.5 fgedha ambazo
zimepelekea ujenzi wa Maabara ya Afya ya Jamii pamoja na ununuzi wa vifaa
tiba,” alisema Dk. Subi.
Aidha Dk. Subi alisema kuwa katika mwaka wa fedha
2023/2024, hospitali hiyo iliwahudumia jumla ya watu 36,154 na
kwamba asilimia 90 ya wananchi wanaofika kutibiwa katika hospitali wanaridhika
na huduma zinazotolewa na hiyo.
Aliongeza kuwa “Asilimia 75 ya wagonjwa waliotibiwa ugonjwa Kifua
Kikuu Sugu (TB) wamepona na haya ni mafanikio makubwa ikilinganishwa na kiwango
cha mataifa cha asilimia 63 ya wale waliopona baada ya kupata matibabu”,
alisema.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Bodi uliomaliza muda wake,
Mjumbe wa bodi hiyo (iliyomaliza muda wake) Daniel Sendewa aliishukuru Serikali
kupitia Wizara ya Afya kwa kuwaamini jambo ambalo limepelekea hospitali hiyo
kupata mafanikio makubwa.
“Nichukue fursa hii pia kuishukuru Serikali kwa ushirikiano wake
mkubwa kwa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH)
ambao umeifanya hospitali hii kupata heshima ndani na nje ya nchi”, alisema
Sendewa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo ambayo ni ya tatu
hospitalini hapo, Prof. Muhammad Bakari Kambi aliishukuru Serikali kwa
kuwaamini na kisha kuwakabidhi jukumu la kushirikiana na uongozi wa KIDH kwa
ajili ya kuboresha sekta ya afya.
Aidha aliupongeza uongozi wa bodi iliyomaliza muda wake kwa kazi
nzuri zilizopelekea KIDH kustawi na hali iliyopelekea (KIDH) kuwa uendelevu, na
hivyo kupelekea uteuzi na hatimaye uzinduzi wa bodi mpya.
Miongoni mwa Wajumbe wa Bodi hiyo walioteuliwa na Waziri wa Afya ni pamoja na Dk. Mary Mayige,
Adelmarsi A. Ndangasani, Dk. Stanley P. Chattanda, Mauldid N. Nyamlenganwa,
Prof. Kajiru G. Kajiru na Dk. Ntuli Kapologwe.