Maabara ya Usalama wa Kibaiolojia Kibong’oto, kuimarisha Tiba na Utafiti wa Magonjwa Ambukizi


Mkurugenzi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH), Dkt. Leonard Subi.

SIHA-KILIMANJARO.

Uongozi wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH), umesema uwepo wa Maabara ya Usalama wa Kibaiolojia Daraja la Tatu, utachangia katika udhibiti wa kusambaa kwa mgonjwa duniani na hivyo kuimarisha uchumi na usalama wa binadamu.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt. Leonard Subi, aliyasema hayo hivi karibuni, wakati akiwasilisha taarifa ya hospitali hiyo kwa Waziri wa Afya Jenista Mhagama alipotembelea hospitalini hapo.

Dk. Subi alisema Ujenzi huo wa Maabara hiyo ulifanyika kwa awamu mbili na uligharimu Sh Bilioni 22.5 zinazojumuisha ujenzi pamoja na ununuzi wa vifaa tiba.

“Maabara hii itafanya ufuatiliaji wa usugu wa vimelea kwa dawa zinazotumika kwenye matibabu ya magonjwa mbalimbali, uchunguzi wa ufanyaji kazi ini, figo, homoni, uchunguzi wa vimelea vya magonjwa vyote ikiwemo njia za kimoleculi na kufanya tathimini ya kiwango cha dawa mwilini ili kuboresha matibabu,”alisema Dk. Subi.

Akizungumzia kuhusu utafiti Dk. Subi alisema kwamba maabara hiyo itatumika pia katika tafiti mbalimbali na ubunifu (innovation) katika Sayansi ya tiba na kinga katika ugunduzi wa dawa, vitendanishi, vifaa tiba pamoja na kuwezesha kutengeneza chanjo na vitendanishi mbalimbali za kuzuia na kukinga magonjwa ambukizi huko mbeleni.

Alisema maabara hiyo ina uwezo mkubwa pia wa kuhifadhi sampuli za vimelea vya kwa muda mrefu hadi miaka 50 na uwezo wake wa kuhifadhi ni lita 47,000, na kusema kuwa ni moja ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Maabara yetu imepata vifaa vya kisasa kabisa vya zaidi ya Sh bilioni 10 ikiwemo kuchakata vimelea na vinasaba na hivyo kubainisha chanzo cha maradhi na ufuatiliaji wake ikiwemo magonjwa ya milipuko na kwamba maabara hiyo itatumika kwenye mafunzo na kujenga uwezo wa wataalam wetu pamoja na wanafunzi.”alifafanua.

Aidha Dk. Subi alisema KIDH ilikuwa ni hospitali ya kwanza Tanzania kuweza kubainisha anuai za Covid-19, ambapo walipokea sampuli 69 kutoka Wizara ya Afya na kwamba kifaa cha kwanza kilichotumika kuchunguza anuai hizo kilifanyika chini ya Mwanasayansi mahiri Dk. Shaban Mziray, kutoka Kibong’oto.

Aliongeza kuwa maabara hiyo inatarajia kuboresha huduma za tiba, kupunguza gharama ambazo serikali inaingia katika kupeleka sampuli nje ya nchi kwa uchunguzi.

Katika hatua nyingine Dk. Subi alisema hospitali ya Kibong’too kupitia Maabara yake ya Afya ya Jamii imechaguliwa kujengewa uwezo ili kuwa na hadhi ya juu ya rufaa ngazi ya kimataifa yaani Supra National Lab na kuwa maabara ya tano huku ikiongoza katika utafiti wa kupunguza muda wa matibabu kwa wagonjwa wa TB katika nchi 6 za Afrika.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.