MOSHI-KILIMANJARO.
Serikali imewataka
mafundi rangi na ujenzi mkoani Kilimanjaro, kuutumia mfumo wa ununuzi wa
kielektroniki wa (Nest),ili kuomba kazi za ujenzi zinazotangazwa na
halmashauri.
Rai hiyo imetolewa jana
na Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi mkoani humo Shaban Mchomvu, wakati
akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa Chama cha Mafundi Rangi na Ujenzi
(CHAMARUKI),uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Morio Hall mjini Moshi
mkoani humo.
Mchomvu alisisitiza
kuwa nidhamu, upeo wa kuziendea fursa hasa kupitia mitandao na majukwaa
mbalimbali ni jambo muhimu kwa mafundi ili kufanikisha kazi zao na kujikwamua
kiuchumi.
Aliwataka mafundi hao,
kuhakikisha kwamba wanautumia mfumo wa ununuzi wa kielektroniki (NeST) kwa
udailifu, uwazi na uwajibikaji ili kunufaika na fursa za ujenzi zilizopo ndani
ya serikali na taasisi binafsi katika kufikia malengo yao.
“Rais Samia ameleta
fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo katika mkoa wetu wa Kilimanjaro, hata
kama mkiamua leo hii kuigawana kuna miradi mingine mtaiacha, hivyo niwasisitize
suala la nidhamu ya matumizi mazuri ya mitandao,”alisema Mchomvu.
Alisema kuwa umoja
miongoni mwa mafundi ni jambo muhimu sana na kwamba kupitia umoja huo aliutaka
uongozi wa CHAMARUKI kuhakikisha wanawahamasisha mafundi wanawake kujiunga na
chama hicho ili kufikia malengo tarajiwa zikiwemo fursa za ujenzi.
Awali akizungumza
Katibu Chama cha Mafundi Rangi na Ujenzi (CHAMARUKI), mkoani humo Casmiry John
Toto, alisema wameanzisha chama hicho kwa lengo la kutengeneza thamani ya
mafundi katika jamii na kuziendea fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi kupitia
umoja wao.
“Tunatengeneza sauti
ya kuweza kuwasilisha jambo ambalo linaweza kuwa na tija katika jamii, kuondoa
dhana ya kuiona sekta ya ujenzi ni kama sekta ya watu ambao hawana, lakini pia
ni sehemu ya kupaza sauti kwa maslahi mapana kwa jamii na taifa kwa
ujumla.”alisema Toto.
Kwa upande wake Meneja
wa tawi la Azania Benk Moshi Moshi, mkoa wa Kilimanjaro Yusuf Lenga;
aliwapongeza kwa kuanzisha umoja huo huku akisema kuwa sekta ya ujenzi
(mafundi) ni sekta muhimu katika maendeleo hapa nchini.
“Sekta ya
mafundi rangi na ujenzi ni sekta ambazo zinabadilisha maisha,
mtizamo na hali za Watanzania na Taifa kwa ujumla hivyo nawapongeza sana kwa
kuanzisha umoja wenu huu.”alisema Lenga.
Aliongeza kuwa “Sisi
Azania Benk tunaona umuhimu wa kushirikiana na (CHAMARUKI), kama sehemu
ya jamii, tunato huduma mbalimbali ikiwemo mikopo ya kimaendeleo kwa mafundi
mmoja mmoja na vikundi ambao wanaotambulika na serikali.”alisema.
Yusuph Said na Judika Evarest ni baadhi ya mafundi wanaounda umoja huo walielezea matumaini yao ya umuhimu ya kuwa na chama hicho katika kuzifikia fursa zilizopo, ambapo katika mkutano huo pia ulihudhuriwa na wafanyabiashara na wadau mbalimbali waliopo katika sekta ya ujenzi ambapo pamoja na mambo mengine wajumbe hao, walipitisha rasimu ya mapendekezo ya Katiba yao sambamba na kusomewa taarifa ya mapato na matumizi.









