MOSHI-KILIMANJARO
Kampuni ya Magic Builder's
International Ltd, inayojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za ujenzi kama vile
white skim wall putty, imejizatiti kuwalipia ada watoto wa mafundi rangi na
ujenzi wanaosoma shule za msingi za serikali.
Hayo yamesemwa na Afisa Masoko wa
Kampuni hiyo Kanda ya Kaskazini, Brighton Geofrey, katika mkutano mkuu wa Kwanza wa Chama cha Mafundi Rangi na Ujenzi (chamaruki),uliofanyika Morio Hall mjini Moshi,
mkoani Kilimanjaro.
Geofrey alisisitiza kuwa hatua
hiyo ni sehemu ya kutambua mchango wa mafundi rangi na ujenzi ambao ni wadau
muhimu katika kufanikisha malengo ya kampuni hiyo.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo
imekuwa ikiunga mkono juhudi za serikali za kuboresha miundombinu ya elimu,
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa mapya na urekebishaji wa yale ya zamani.
Kwa upande mwingine, alielezea
kuwa kampuni hiyo ina mipango ya kuendelea kusaidia mafundi rangi na ujenzi, na
kwamba wameanzisha mpango huu katika mkoa wa Kilimanjaro kama sehemu ya
michango yao kwa jamii.
Vilevile, aliwashauri mafundi hao
kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kujisajili kwenye mfumo wa Nest wa
serikali ili kupata fursa za kazi kupitia makampuni ya vifaa vya ujenzi.
Katika hatua nyingine, kampuni hiyo pia imetangaza kuwa itaendelea kutoa zawadi kupitia bahati nasibu kwa mafundi mbalimbali katika mikoa mbalimbali nchini.





