Waziri wa Afya; Januari 10,2025 kuizindua Bodi mpya ya Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto


KIBONG’OTO-SIHA.

Waziri wa Afya Jenista Mhagama, kesho (Ijumaa) anatarajiwa kuizindua Bodi mpya ya Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto.

Hayo yameelezwa Januari 9,2025 na Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk. Leonard Subi, wakati akizungumza na Kisena Blogspot Ofisni kwake, ambapo alisema Bodi mpya iliteuliwa tangu Oktoba 2024 na itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu hadi Oktoba mwaka 2027.

“Bodi kama mnavyofahamu inasimamia uendeshaji wa hospitali, hususan katika masuala mazima ya kuwa na Sera, mpango mkakati wa hospitali unavyotekelezwa kama jinsi ulivyopangwa, kusaidia utafutaji wa rasilimali fedha, utekelezaji wa mpango wa kila mwaka na mambo mengine”, alisema Dk. Subi.

Akizungumzia Bodi iliyomalizia muda wake, Dk. Subi alisema bodi hiyo chini ya uenyekiti wa Dk. Said Egwaga, ilifanya mambo mengi jambo ambalo limechangia hospitali hiyo kupiga hatua kubwa na kupata mafanikio ndani na nje ya nchi.

Akielezea mafanikio hayo, Dk. Subi, alisema ni pamoja na ujenzi wa jengo la wagonjwa mahtuti hospitalini hapo lenye vitanda 20 ambapo alisema limejengwa kwa fedha za UVIKO-19  jengo ambalo ni la kwanza kujengwa hospitalini hapo.

Alisema “Umuhimu wa jengo hili ni kuwa litauwezesha uongozi wa hospitali kuokoa maisha ya wagonjwa wengi kwa vile itakuwa na vifaa vya kisasa vinavyohitajika kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa ambao hali yao imekuwa mbaya sana”, alisema DK. Subi.

Alifafanua kuwa fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 zilizoanzishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zimeendelea kuzaa matunda mazuri, ambapo zimewezesha kujenga mradi wa jengo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) na kugharimu kiasi Sh bilioni 1.3.

“Tangu hospitali hii ianzishwe miaka 99 iliyopita, haijawahi kuwa na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), kitengo ambacho ni muhimu sana linapokuja suala la kutoa matibabu hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba, matibabu tunayotoa hapa ni mahususi kwa magonjwa ya kuambukiza kikiwemo Kifua Kikuu (TB)”, alisema Dk. Subi.

Aliongeza kuwa Serikali imetumia Sh milioni 727 kwa ajili ya kununulia vifaa vinavyohitajika katika ICU mpya ambayo ina vifaa vyote muhimu vinavyohitajika ikiwemo mifumo yote ya hewa ya Oxgen ambayo ni muhimu sana kwa wagonjwa walio katika hali mahtuti.

Alisema mradi huo pia ulihusisha kuweka mfumo wa umeme, mfumo wa tiba ya oksijeni, mfumo wa IT, mfumo wa maji safi na ukarabati wa mazingira ya nje ya hospitali hiyo.

Dk. Subi akazungumzia vifaa vilivyonunuliwa na serikali kwa ajili ya kitengo hicho kipya ni pamoja na vitanda 10 maalum kwa ajili ya wagonjwa wa ICU, mashine 10 za kupumulia, mashine  10 za kufuatilia wagonjwa, Defibrillator moja, vifaa vya Ultrasound, Suction Machine pamoja na vifaa vingine vya matibabu vinavyohitajika katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Alisema kuwa Serikali pia imejenga jengo la kutoa huduma za uchunguzi kwa njia ya mionzi hospitalini hapo lenye thamani ya Sh bilioni 3.4 ambapo kwa sasa huduma zinazohusiana na uchunguzi kwa njia ya mionzi zinapatikana hospitalini hapo.

Alisema uongozi wa hospitali hiyo; umeanzisha huduma kwa kutumia gari maalum lenye vifaa vya kisasa vya teknolojia ya juu ambayo limesaidia kuwafikia wagonjwa wengi na hata wale walioko katika Mikoa mingine nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.

“Kwa kutumia mobile clinic, tumeweza kugundua wagonjwa wengi walioko nje ya Kilimanjaro, ikiwemo kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo wamepata huduma ambazo wasingeweza kuzipata kutokana na umbali ulioko kati ya maeneo yao kijiografia na hospitali ya Kibong’oto iliko”, alisema. 

Dk. Subi alielezea mafanikio mengine yaliyopatikana hospitalini hapo kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuweko kwa watumishi waliobobea katika kutoa huduma katika sekta ya afya ikilinganishwa na pale taasisi hiyo ilipoanzishwa.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.