ROMBO-KILIMANJARO.
Serikali kupitia
Wizara ya Afya imetenga fedha Sh bilioni 1 katika Bajeti ya Mwaka 2024/25 kwa
ajili ya kujenga chuo cha uuguzi Wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Afya Jenista
Mhagama aliyasema hayo Januari 7,2025 Wilayani Rombo, wakati akiwa katika ziara
ya siku mbili mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kukagua na kuzindua miradi ya
Sekta ya Afya katika Wilaya ya Rombo pamoja na Wilaya ya Same.
Alisema Serikali
imetenga zaidi ya Sh bilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo hicho,
ambacho kitajengwa wilayani Rombo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.
Waziri Mhagama, alisema
ujenzi huo unaratajiwa kuanza mwezi Machi mwaka huu, ili kupunguza tatizo la
watumishi wa kada ya afya na chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kuchukua vijana
takribani 600 huku vijana watakao kuwa wakiishi kwenye mabweni ni 400.
“Serikali imeona ipo
haja ya kuongeza idadi ya wataalam wa Afya kwa kujenga Chuo cha uuguzi ili
kuboresha upatikanaji wa wataalam wa afya nchini.”alisema Waziri Mhagama.
Aidha Waziri Mhagama,
alisema ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Serikali
ilitoa Sh bilioni 82 katika Wilaya Rombo, ili kutekeleza miradi mbalimbali
ikiwemo miradi ya afya.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliishukuru Serikali huku akisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ra Rais Samia madarakani, mkoa ulipokea Sh bilioni 956 za miradi ya maendeleo.
