KOROGWE-TANGA.
Wakazi wa Wilaya ya Korogwe na Lushoto
Jijini Tanga, wameipongeza
Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) kwa kuanza kuchukua hatua za kuweka lama
za kudumu za utambuzi wa maeneo yenye vyanzo vya maji ili kuvinusuru
na uharibifu unaosababishwa na shughuli za kibinadamu.
Akizungumza mmoja wa wakazi
wa wilaya hiyo James Kaniki, alisema serikali kuanza kuchukua hatua za utambuzi
wa maeneo yenye vyanzo vya maji na kuweka alama ni jambo zuri, kwani itasaidia
kuvilinda vyanzo vya maji ili kuendelea kuwa na uhakika wa maji safi na salama
wakati wote.
“Hatu za Bodi ya Maji Bonde
la Maji Pangani, kuweka alama za kudumu zitasaidia sana kuzuia shughuli za
kilimo na ufugaji ambazo zinaathiri kwa kiwango kikubwa maeneo yenye vyanzo vya
maji,”alisema Kaniki.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji
Bonde la Pangani Mhandisi Segule Segule; alisema kufuatia uvamizi wa vyanzo vya
maji PBWB, imeanza shughuli ya tathmini
ya vyanzo ili kuweka alama za mipaka (beacons), kwa kushirikiana na viongozi wa
Kata na Kijiji ili kuweza kuhifadhi chanzo cha Kwematambwe ambacho kimevamiwa
na shughuli za kibinadamu pamoja na Mto Umba.
Mhandisi Segule, alisema Sheria
za Usimiamizi wa rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2001 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 20 ya mwaka
2004 kifungu namba 57 ambacho kinakataza shughuli za binadamu ndani ya mita 60
kwenye vyanzo vya maji.
Akizungumza kwenye kikao
cha tatu cha wadau wa Usimamizi wa rasilimali za maji kidakio cha Mto Umba
Segule alisema Mkoa wa tanga una vyanzo vya maji zaidi ya 400 huku vyanzo 140
pekee ndio vyenye mipaka ya alama za utambuzi, ikiwa ni jitihada za
kuwachukulia hatua za kisheria wananchi ambao wanatumia huduma za maji bila
vibali maalum hali ambayo inasabisha uharibifu wa miundombinu .
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Korogwe William Mwakilema,aliwataka wananchi na wadau wote wa
rasilimali za maji kufuata Sheria na kushirikiana na Bodi ya maji Bonde la
Pangani kuendelea kutunza vyanzo vya maji.
“Ni kosa la mwananchi
yeyote kuchepusha maji au kutumia maji pasipo kuwa na vibali maalum na adhabu
inayotolewa ni kifungo cha miaka miwili hadi mitano jela na kiasi cha Sh laki 5
hadi milioni 50.”
Bodi ya Maji Bonde la
Pangani inasimamia eneo bonde lenye ukubwa wa takribani kilomita za mraba
54,600 ambayo ni asilimia 93% ya Bonde zima na asilimia 7 iko Nchini Kenya
inayolifanya Bonde la Pangani kuwa ni la kimataifa.
Pia Bodi ya Maji Bonde la
Mto Pangani inasimamia Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara katika
Halmashauri za Wilaya takribani 24.





