Majengo 24,119 kufanyiwa mapitio ya uhakiki Kilimanjaro

HAI-KILIMANJARO

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, inakusudia kufanya mapitio ya uhakiki wa majengo 24,119 yaliyokuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi mkoani Kilimanjaro.

Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Wizara Suleiman Mvunye, aliyasema hayo Januari 7,2024, wakati akitoa maelezo ya utangulizi katika hafla ya ufunguzi wa kikao cha uhakiki wa taarifa za anwani za makazi, kilichofanyika wilaya ya Hai mkoani humo.

Mvunye ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mohamed Khamis Abdullah, kwenye kikao hicho, alisema tayari uhakiki umeshafanywa katika wilaya 35 zilizoko Tanzania Bara, Zanzibar na Pemba.

Alisema Wizara imeona kuna muhimu wa kufanya mapitio ya uhakiki wa majengo hayo, ili yaweze kuorodheshwa kwenye mfumo wa anwani za makazi, kutokana na kupita kwa takribani miaka mitatu tangu oparesheni ya anwani za makazi kufanyika mwaka 2022.

Awali akizungumzia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Dionis Myinga, alisema mafunzo hayo yatafanyika kwa siku mbili yakiwashirikisha Wenyeviti na Watendaji wa Kata, Mitaa pamoja na Watendaji wa Vitongoji na Vijiji, wilayani humo na kwamba imelenga kuwajengea uwezo washiriki hao uwezo wa kushiriki zoezi la uhakiki wa anwani za makazi ambapo alisema uelewa wao utawezesha zoezi hilo kuwa endelevu na hivyo kurahisisha shughuli za kimaendeleo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Edmund Rutaraka, alisema uhakiki huo wa anuwani za makazi, utawezesha malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ambayo imejiwekea kuweza kufikiwa.

Akifungua semina hiyo Mkuu wa Wilaya ya Hai Lazaro Twange, aliwataka wananchi wilayani humo,  kutoa ushirikiano wao wakati wa uhakiki wa taarifa za anwani za makazi kutokana na umuhimu wa zoezi hilo kwa maendeleo ya Taifa.

Twange alisema zoezi hilo lina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa kwani matokeo yake yanatoa takwimu zinazohusiana na idadi ya watu na makazi yao kwa ujumla na hivyo kuwa dira nzuri kwa Serikali kutekeleza shughuli za maendeleo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Suleiman Mvunye, akitoa maelezo ya utangulizi katika hafla ya ufunguzi wa kikao cha uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Mkuu wa Wilaya ya Hai Lazaro Twange, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi kwa Wilaya hiyo, kikao kilichowashirikisha Wenyeviti na Watendaji wa Kata, Mitaa, Watendaji wa Vitongoji pamoja na Vijiji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Dionis Myinga.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.