NDUNGU-SAME
Waziri wa ujenzi Abdallah Ulega amemtaka mkandarasi aliyepewa jukumu la kujenga sehemu ya pili ya ujenzi wa barabara ya Ndungu-Mkomazi yenye urefu wa kilomita 36 kwa kiwango cha lami, kuhakikisha barabara hiyo anaijengwa kwa kiwango cha kimataifa kama inavyotarajiwa.
Waziri Ulega, alitoa maagizo hayo
Januari 4, 2025 Wilayani Same mkoani Kilimanjaro, wakati wa hafla ya kumkabidhi
mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kutoka Kampuni ya China Communications
Construction Company Limited, eneo la kazi kwa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo,
tukio lililofanyika Kata ya Ndungu Wilayani humo.
Waziri Ulega alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha kwamba ujenzi
wa barabara hiyo unazingatia thamani ya fedha za mradi na kwamba Serikali haita
sita kuwachukulia hatua kali za kisheria pale ambapo watabainika kwenda kinyume
na mikataba ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Napenda kusisitiza kuwa gharama ya ujenzi wa Barabara hii ni kubwa
hivyo tuzingatie thamani ya fedha ya Mradi (Value for Money) wakati wa ujenzi.”alisema
Aidha Waziri Ulega, alitoa
maagizo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Balozi Aisha Amour, Mtendaji Mkuu wa
TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, Mhandisi Msimamizi wa Ujenzi Tanroads, na
Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Motta Kyando, kuhakikisha
wanamsimamia vyema mkandarasi huyo ili kazi hiyo ikamilike kwa kiwango ambacho
kinatarajiwa na Watanzania ambao ndiyo walipa kodi wa wakuu.
“Kama kuna kitu ambacho Rais Samia Suluhu Hassan anakichukia ni
pale anapoona fedha nyingi za umma zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara halafu
baada ya mwaka mmoja, barabara inaanza
kukarabatiwa; hayo ni matumizi mabaya ya fedha za umma na ambayo sisi wasaidizi
wa Rais hatutavumilia kuona yakitokea”, alisema Waziri Ulega.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa batabata hiyo kwa kiwango cha
lami, awamu ya pili, Waziri Ulega alisema barabara hiyo inatarajiwa kugharimu kiasi
cha Sh Bilioni 59.7 na kwamba kukamlika kwake kutawaondolea wananchi wa Same
adha ya usafiri inayotokana na miundombinu ya barabara isiyo rafiki waliyokuwa
wakiipata kwa miaka mingi.
“Kukamilika kwa barabara hii wananchi hawa watanufaika kwa
kusafirisha mazao ya kibiashara ikiwemo chakula ambayo yatakuwa yanafika sokoni
mapema ikilinganishwa na hali ilivyo sasa”, alisema.
Pia alisema barabara hiyo itakwenda kuwarahisishia usafiri kwa
ajili ya shughuli za kiafya na kijamii, sambamba na kushuka kwa gharama za
usafiri kutokana na ukweli kutakuwa na vyombo vingi vya usafiri kutokana na
kuweko na miundombinu bora ya barabara.
“Kukamilika kwa barabara hii, itachangia kukua kwa sekta ya
utalii Wilayani Same kwa vile miundombinu mizuri ya barabara hiyo itaongeza
idadi ya makampuni ambayo yatawapeleka watalii kutembelea hifadhi ya Taifa
Mkomazi”, alisema.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tanroads Mhandisi Mohamed
Besta, alisema kuwa makabidhiano hayo yanahusu sehemu ya pili ya barabara ya
Ndungu-Mkomazi yenye urefu wa kilomita 36.
Alisema awamu hiyo ya pili ya ujenzi wa barabara ya
Ndungu-Mkomazi ni muendelezo wa ujenzi wa barabara ya Same-Kisiwani-Mkomazi yenye
urefu wa kilomita 100.5 kwa kiwango cha lami.
“Baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, mnamo
mwaka wa 2021, Serikali ilielekeza kuanza kwa ujenzi wa awamu ya kwanza kwa
kiwango cha lami ambao ulihusisha kilomita 5.2 kati ya Mroyo na Ndungu”,
alisema.
Aliongeza, “Serikali kupitai Wakala wa Barabara nchini Tanroads
Mkoa wa Kilimanjaro iliingia mkataba na Kampuni ya kizalendo ya Bona and Hubert
Engineering Limited; utekelezaji wa awamu hiyo ya kwanza umefikia asilimia 72
ambapo unatarajiwa kukamilika Januari 31, mwaka huu”, alisema.
Alisema mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali, unaolenga
kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwenye Mikoa ya Kilimanjaro na
Tanga hususan katika Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro na Korogwe, mkoani
Tanga.
Mhandisi Besta aliendelea kusema kuwa barabara hiyo ni moja kati
ya mitandao ya barabara muhimu katika Mkoa wa Kilimanjaro na Tanga ambapo kuna
maeneo ambayo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga na tangawizi, ambayo ni baadhi
ya mazao muhimu ya kibiashara.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, alisema atahakikisha barabara hiyo serikali inaisimamia ili iweze kujengwa na kukamilika ndani ya mkataba wa kazi.















