MOSHI-KILIMANJARO
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, amekabidhi msaada wa chakula kwa vituo sita vya watoto waishio mazingira magumu mkoani humo, ikiwa ni ishara ya kushirikiana nao katika kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya.
Babu alikabidhi zawadi hizo Januari Mosi mwaka huu, kwa niaba ya Rais Samia, ambapo alisema kuwa Rais amekuwa na utaratibu wa kutoa zawadi hizo kwa ajili ya kuungana na watu wenye mahitaji maalumu kusherehekea Sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya.
“Rais Samia
amekuwa na utaratibu wa kutoa zawadi kwa
watoto wote waishio katika mazingira magumu wakati wa Sikukuu zote kubwa hapa
nchini,”alisema Babu.
Mkuu huyo wa
mkoa alisema misaada hiyo ambayo Rais Samia amekuwa akiitoa ni ishara ya
kuendelea kuwakumbusha Serikali inawajali, inawathamini na kuwapenda hivyo
wasijione wanyonge au kutengwa na jamii.
"Nipo hapa
mbele yenu kwa niaba ya kuwaletea salamu kutoka kwa Rais Dk. Samia Suluhu
Hassan, ambaye amenituma kuja kuwakabidhi zawadi za Sikukuu ya Krismasi na
Mwaka Mpya.”alisema. RC Babu.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Jairy Khanga, alisema zawadi hizo ni pamoja na mchele kilo 600, unga wa ugali kilo 300, sukari kilo 300, mafuta ya kupikia lita 120, sabuni ya unga mifuko 18, maji na soda katoni 10, pampasi na taulo za kike boksi mbili.
Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa vituo hivyo vilivyokabidhiwa zawadi hizo Mkurugenzi wa Programu wa Amani Centre, Daniel Temba, alisema wanatambua mchango wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuguswa na watu wa makundi maaluumu.





