SAME-KILIMANJARO.
Waziri wa Maliasili na
Utalii Balozi Dk. Pindi Chana, ameipingeza
Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB),kwa juhudi zao za kutunza vyanzo vya maji
na maliasili zilizopo nchini.
Dk. Chana alitoa pongezi hizo hivi karibuni, akiwa Wilayani
Same mkoani Kilimanjaro, wakati akifungua Msimu wa Pili wa
Tamasha la Utalii Same, ambapo alisema
ufanisi wa Bodi hiyo, umewezesha rasilimali za maji kutunzwa kwa njia endelevu
na hivyo kuleta manufaa kwa jamii na mazingira kwa ujumla.
Waziri Chana, alitaja
juhudi za viongozi hao katika kukuza sekta ya utalii kama mfano mzuri wa
ushirikiano na uongozi bora, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea na juhudi
hizo, ili kudumisha ustawi wa mazingira na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi
na salama kwa vizazi vijavyo na kwa maisha ya wanyama.
Aidha Waziri Chana,
aliwataka wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, kuhakikisha wanaunga mkono jitihada
zinazofanywa na Bodi ya Maji Bonde la Pangani kwa kuvitunza vyanzo vya maji na
kusema kuwa Serikali haitamuacha salama mtu yeyote atakayehusika na kuharibu vyanzo
vya maji.
Akizungumza kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani, Afisa Maendeleo ya Jamii Bodi ya
Maji Bonde la Pangani (PBWB), Patrice Otieno, alisema kuwa kutokana na elimu
ambayo imekuwa ikitolewa na Bodi, baadhi ya wananchi wameanza kupata uelewa na
kuanza kuchukua hatua muhimu katika kuhifadhi vyanzo vya maji.
“Tunafahamu matumizi ya
maji ni mengi sana hususani kwa wakulima ambao hutumia maji mengi kwa ajili ya
kilimo na umwagiliaji, lakini tumekuwa
tuhakikisha maji haya pia yanatiririka kwenda kwenye mbuga ili wanyama
na mimea iweze kupata maji pia.”alisema Otieno.
Aidha Otieno, alisema Bodi ya Maji Bonde la Pangani, itaendelea kuhakikisha kwamba maeneo yote yenye vyanzo vya maji kuanzia kwenye milima, mabonde, mito, maziwa na chemichem, zinaendelea kuwa na maji kwa kuyahifadhi, ikiwa ni sambamba na kupanda miti kwa wingi pamoja na kuweka mabango yyenye makatazo ya kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60.





