MKOMAZI-SAME.
Baadhi ya wagonjwa
waliotibiwa, Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH)
iliyoko Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, wameipongeza Serikali kwa kuchukua
jukumu la kulipia gharama za matibabu ya Kifua Kikuu hospitalini hapo.
Wagonjwa hao walitoa
shukrani hizo jana, wakati wa ziara ya siku moja katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi, iliyoko Wilaya ya Same mkoani humo, iliyoandaliwa na uongozi wa hospitali hiyo, ambapo
walisema uamuzi huo wa Serikali kuwagharamia matibabu yao, umewawezesha kuokoa
maisha yao kutokana na ukweli kuwa gharama za matibabu ya ugonjwa huo ni kubwa
sana.
Akizungumza mmoja wa
wagonjwa waliotibiwa Kifua Kikuu Sugu (TB), hospitalini hapo na kupona kabisa Ally
Seif Salim alisema “Mbali na huduma za matibabu kuwa ni za juu sana, pia Serikali
inagharamia vipimo kabla ya kuanza matibabu, chakula na mavazi wakati wa
kipindi chote cha matibabu ambacho ni kirefu sana”,alisema.
“Wakati nilipoletwa katika
hospitali ya Kibong’oto hali yangu ilikuwa mbaya sana, kiasi cha kupoteza
matumaini yangu ya kuishi, lakini kwa sasa nimepona kabisa.”alisema.
Mnufaika mwingine Hansibari
Ally Mvita kutoka mkoa wa Lindi, alisema baada ya kusumbuka na TB kwa muda mrefu,
hatimaye aliletwa hospitali ya Kibong’oto na kuanza kupatiwa matibabu ambayo
yalimwezesha kupona kabisa.
“Nilikuwa nikisumbuliwa na maumivu
ya kifua kwa miaka mingi sana na nilihangaika kwa muda mrefu haswa kwenye tiba za
asili; hali ilipofikia kuwa mbaya, baada ya kuanza kutapika damu nilipekwa
hospitali ya Nachingwea na kugundulika nilikuwa na ugonjwa wa Kifua Kikuu Sugu
(TB),”, alisema Mvita.
Alisema baada ya
kugundulika kuwa na TB Sugu, alipatiwa rufaa ya kuletwa hospitali Maalum ya
Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto na kuanzishiwa matibabu chini ya ufadhili wa
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia na sasa nimepona.
Kwa upande wake mnufaika
mwingine Husna Sabato kutoka Musoma mkoa wa Mara, ambaye alibainika
kuwa na TB Sugu, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha kugharamia matibabu yake na
kuweza kupona kabisa ugonjwa huo, bila kutumia gharama zozote.
“Ninaushukuru sana uongozi
wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH), chini ya Mkurugenzi wake Dk. Leoinard Subi, kwa namna
inavyojitahidi kwa kila hali kuhakikisha Kifua Kikuu Sugu kinatokomezwa kwa
watu wazima na watoto.”alisema.
Akizungumiza safari ya
kutembeleea hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mvita alisema amefarijika sana kuwaona
wanyama aina ya Faru weusi na Mbwa Mwitu,
wanyama ambao hakuwahi kuwaona na kwamba ziara ya mbugani imemuondolea
mawazo ya kukaa kwenye tiba kwa muda mrefu jambo ambalo alisema pia lilimfanya kuwa
mbali na familia yake kwa muda mrefu na kujihisi kwamba ametengwa.
Akizungumzia safari hiyo, Afisa Ustawi wa Jamii Hospitali Maalum ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto Wazoeli Mshana, alisema uongozi wa (KIDH), ulianzisha programu hiyo tangu mwaka 2022 ya kuwapeleka mbuga za wanyama wagonjwa wa Kifua kikuu waliotibiwa na kupona ili kuwafariji kutokana na kukaa kwenye matibabu kwa muda mrefu.
“Wagonjwa hawa huwa wengi
wao wanatoka nyumbani kwao kuja kwa matibabu na hukaa kwa muda mrefu, kati ya
miezi sita hadi tisa bila ya kutoka hospitalini, hivyo tukaona baada ya kupona
ni vyema wakapata fursa ya kujifariji ndipo tukaja na wazo la kuwapeleka
watembelee hifadhi za Taifa”, alisema.
Akizungumzia uamuzi wa Serikali
kugharamia matibabu ya kifua kikuu, Mshana alisema hatua hiyo ni mkombozi
mkubwa kwa wagonjwa ambao wangelazimika kutumia gharama kubwa sana za matibabu
ya Kifua Kikuu haswa kwa wale ambao wamefikia hatua ya kuwa na ugonjwa wa Kifua
Kikuu Sugu TB.
“Gharama za kumtibu mgonjwa
wa Kifua Kikuu cha kawaida ni kati ya SH milioni 12 na milioni 15, wakati Kifua
Kikuu Sugu (TB), matibabu yake ni kati ya Sh milioni 15 hadi milioni 40 kwa mtu
mmoja; na hii inatokana na mgonjwa kuhitaji kama kukaa hospitalini hapa kati ya
miezi sita hadi tisa ili apone kabisa”, alisema.
Aidha Mshana aliipongeza Taasisi
ya LHL International, kwa
ksuhirikiana na Serikali kulipia baadhi ya gharama za matibabu na mahitaji
mengine kwa ajili ya wagonjwa wa Kifua Kikuu wanaopata tiba hospitalini hapo.
Kwa upande wake Dk. Lilian
Mahemba kutoka kitengo cha Kifua Kikuu Sugu, alisema dhana ya kuwapeleka
waliopona kutembelea hifadhi za Taifa kuna wawezesha kubadili mazingira na pia
kuwaongezea furaha wanazopata baada ya kupona ugonjwa ambao umewasumbua kwa
muda mrefu.
Aidha alitoa ushauri kwa
wananchi wanapojisikia hali tofauti kwenda mara moja kwa wataalam wa afya ili
wakigundulika ya kuwa wanamaradhi ya Kifua Kikuu wapate huduma za mapema ambazo
zitawasaidia kupona kabisa.
Naye Anjela Kimaro kutoka
kitengo cha Fiziotherapia ambacho kinahusika na mazoezi ya upumuaji na viungo kwa wagonjwa
wa Kifua Kikuu, alisema mazoezi hayo huwasaidia wagonjwa kuongeza uwezo wa
kupumua jambo ambalo linawapa unafuu na hivyo kupata nafasi ya kupata tiba na
hatimae kupona kabisa.
“Tunawashirikisha kufanya mazoezi ambayo yatahusisha upumuaji ambayo yatamsaidia mgonjwa wa Kifua Kikuu, kuongeza uwezo wa mapafu kuweka hewa zaidi na kutanua mapafu zaidi ili hewa iweze kukidhi mahitaji ya mwilini”, alisema.




















