SAME-KILIMANJARO.
Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa msaada wa chakula, sabuni na vifaa vingine muhimu kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea wilayani Same, mkoani Kilimanjaro hivi karibuni.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga, amekabidhi misaada hiyo kwa wahanga wa mafuriko hayo kwa niaba ya Rais Samia, ambapo hafla ya kukabidhi misaada hiyo iliyofanyika katika Kata ya Maore, Wilayani Same mkoani humo.
Naibu Waziri Nderiananga alisema mbali na michango hiyo, Rais pia aliagiza Wataalamu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Wilayani humo, kufanya tathmini ya haraka na kuishauri serikali nini cha kufanya ili kuepuka athari hizo kujirudia hapo baadaye.
Aidha Naibu Waziri Nderiananga, aliiagiza Halmashauri hiyo, kutenga bajeti ya kukabiliana na maafa sanjari na kuyabainisha maeneo hatarishi ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari za kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokea zaidi.
Pia; aliagiza kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kinawapelekea wananchi hao mbegu za mahindi na mpunga haraka ili kurejesha mazao ambayo yalisombwa na mafuriko hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni, alisema kuwa jumla ya nyumba 34 zimeharibiwa kabisa na hazifai tena kwa makazi ya watu na zaidi ya ekari 200 za mazao zimeharibiwa na mafuriko hayo ambapo alisema kata za Bombo Kata za Mtii, Vuje, Lugulu na Maore ndizo zilizoathirika zaidi.
Akizungumza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Same Miryam Mjema, alimshukuru Rais Samia, kwa kutoa msaada wa chakula na mahitaji mengine kwa waathirika wa mafuriko ya mvua za vuli zilizonyesha usiku wa Disemba 23, mwaka jana na kuathiri zaidi ya kata tano na kwamba misaada hiyo inalenga kuwapa faraja, furaha, na matumaini wahanga hao.
Awali Diwani wa Kata ya Maore Rashid Juma alisema mbali na nyumba 34 kuharibiwa kabisa, jumla ya nyumba 375 zimeingiliwa na maji katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo na kufanya wahusika kushindwa kuishi ndani.
Katika hatua nyingine diwani huyo; aliishukuru Serikali kwa michango hiyo na kuziomba mamlaka husika kuwapelekea mbegu wakulima wa eneo hilo ili waweze kupanda mazao mapya baada ya yaliyokuwa mashambani kuharibiwa na mafuriko.