Watanzania wahimizwa kufanya utalii wa ndani


MWANGA-KILIMANJARO

Watanzania wamehimizwa kuongeza kasi ya kuvitembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini, ili kuwavutia zaidi watalii kutoka nje ya nchi kuja kuvitembelea.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Kisangara Tours Ltd, Frida Mberesero, ameyasema hayo desemba 28,2024 wakati akizungumza na wana familia zaidi ya 50, waliotembelea hifadhi hiyo kwa ajili ya kujionea vivutio vya utalii vilivyomo katika hifadhi hiyo.

Akiwa katika lango kuu la Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mberesero alisema licha ya uwepo wa vivutio hivyo, bado idadi ya Watanzania wanaofanya utalii wa ndani kwenye vivutio hivyo ni ndogo, ikilinganishwa na idadi ya Watalii wanaotoka nje ya nchi, hivyo ni vema wakaona umuhimu wa uwepo wa vivutio hivyo na kuvitembelea ili kuvutia zaidi watalii kutoka nje.

Mberesero alisema gharama za utalii wa ndani si gharama kubwa kama ambavyo, watu wengi wanavyofikiria na kusema kuwa kutembelea vivutio vilivyopo katika hifadhi hizo ni njia mojawapo ya kuendeleza sekta ya utalii ili kuongeza pato la Taifa na utolewaji wa huduma za kijamii.

Neema Hashim ni miongoni mwa familia ambayo ilitembelea hifadhi ya Taifa Mkomazi, alisema  wamejitolea kuhamasisha utalii  wa ndani, kwakutembelea vivutio mbalimbali kwasababu waanaamini ili kuweza kumshawishi mtu kuhusu vivutio hivyo ni vyema ukawa tayari umefika huko kwanza kwani hiyo inakupa nafasi nzuri yakuelezea uzuri wa ulichokiona.

Mwana familia mwingine Jafari Mberesero, alisema ziara yangu imekuwa yenye mafanikio makubwa sana, sijawahi kumuona Faru akiwa karibu yangu zaidi ya kuwaona kwenye runinga, nimefurahia sana ziara hii ya kutembelea Mkomazi.”alisema.

Naye Elizaberth Kosami,aliwasisitiza Watanzania ni vyema kuendelea kupenda vya kwetu kwa kutembelea vivutio vilivyomo katika nchi yetu na kuondokana na dhana kuwa vipo kwa ajili ya wageni tu kutoka nje ya nchi.

“Uwepo wa mradi wa  Mbwa Mwitu na Faru ndani ya hifadhi ya Mkomazi, umenishawishi kuja mimi na familia yangu, kuwaona wanayama hawa ambao ni adimu kuwaona, ninawasihi Watanzania wenzangu kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini,”alisema Kosami.

Aidha familia hizo zimeishukuru Kampuni ya Kisangara Tours Ltd, kwa huduma zao nzuri wanazozitoa kwani zimewesha,  kutembelea maeneo kadhaa ya utalii ndani yaliyomo ndani ya hifadhi hiyo na kuweza kuwaona wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo Tembo, Nyati, Twiga, Swala, Ndege wa aina mbalimbali pamoja na mradi wa Mbwa mwitu na Faru.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.