Washiriki wa Mafunzo ya Kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria Waomba Wataalam wa Lugha za alama


MOSHI-KILIMANJARO

Washiriki wa Mafunzo ya Kampeni ya huduma za msaada wa kisheria ya Mama Samia, wameomba kwenye Kampeni hiyo kuweko na Wataalamu wa lugha za alama ambao watakwenda kusaidia watu wenye makundi maalum wakiwemo watu wasio na uwezo wa kusikia na kutoa ushirikiano wa kisheria kwao.

Hayo yamejiri wakati wa semina ya mafunzo ya Huduma za Msaada wa Kisheria inayotolewa na Wataalam kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, mafunzo ambayo yameshirikisha wataalam kutoka ofisi za wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Kilimanjaro, maafisa wa jeshi la polisi kutoka dawati la polisi, wasaidizi wa kisheria na mawakili wa kujitegemea.

Akizungumza mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Wakili wa Kijitegemea mkoa wa Kilimanjaro Wilhad Kitaly, alisema ni vizuri kukawepo na Wataalamwa lugha za alama ambao wataweza kusaidia pale watakapopatikana watu wenye changamoto za masuala mbalimbali ya kisheria waweze kusaidia kutatua changamoto hiyo.

Akizungumza kuhusiana na kampeni ya Huduma za Msaada wa Kisheria Wakili Kitaly alisema, “Kampeni hiyo imekuja wakati sahihi kwani hitajio kubwa la wananchi walioko pembezoni wanakabiliwa na changamoto za masuala ya kisheria, kutokana na hali duni za maisha wanashindwa kuwafikia mawakili kwa ajili ya huduma za kisheria kutokana na vipato walivyonavyo.

Naye Afisa ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Siha Joseph Bura, alisema bado watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na Huduma za Msaada wa Kisheria wa Mama Samia hususani wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini.

Alisema changamoto ambazo wanakutana nazo watu wa ardhi nyingi zinatokana na watu kutokuelewa taratibu za kisheria, ziko changamoto ambazo zilitakiwa kupelekwa kwenye baraza la ardhi lakini unakuta zinaletwa ofisi ya ardhi, kuna migogoro ya kifamilia, ambayo inatakiwa kutatuliwa kifamilia lakini unawakuta wanakibilia kuja ofisi ya ardhi.

Awali akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo Mkurugenzi Huduma za Msaada wa Kisheria wa Mama Samia (WAKIS), Ester Msambazi, alisema kampeni hiyo inakwenda kupunguza migogoro, ambayo watakutana nayo wataalam hao katika ngazi za kijamii.

Alisema timu hiyo inatarajia kwenda halmashauri zote za mkoa wa Kilimanjaro, ambapo kila halmashauri watakwenda kata 10, vijiji au mitaa 30 kwa muda wa siku tisa kuanzia Januari 30 hadi Februari 8 mwaka 2025.

Aidha alisema kupitia Kampeni hiyo wamejipanga kuyafikia makundi yote, ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu ili kuweza kupata kundi la watu wenye ulemavu, ambalo litashitriki katika kampeni hiyo.

Akifungua semina hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Nzowa, aliwataka wataalamu hao watakapo maliza mafunzo hayo kwenda kufanya kazi kwa weledi kwa kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zao.

Aidha aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kampeni hiyo ya Huduma za Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, inaotarajiwa kufanyika Januari 30, hadi Februari 8 mwaka huu ambapo huduma hiyo itatolewa kwenye halmashauri zote za mkoa huo.

Semina hiyo imeshirikisha wataalam kutoka ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri, maafisa ardhi, ustawi wa jamii, mawakili wa serikali kutoka halmashauri, maafisa maendeleo ya jamii, maafisa wa jeshi la polisi kutoka dawayi la polisi, wasaidizi wa kisheria na mawakili wa kujitegemea.




 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.