MOSHI-KILIMANJARO
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amewakumbusha Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki na misingi ya utawala bora katika kutekeleza majukumu yao ili kukidhi matarajio ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassam ambaye amewapa dhamana ya uongozi.
Babu alitoa rai hiyo Januari 27,2025 wakati wa hafla ya kumuapisha Mkuu wa mpya wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava iliyofayika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
“Katika kutekeleza majukumu hayo hakikisheni pia mnashirikiana na viongozi wenzenu wa ngazi zote za Wilaya na Mkoa kutokana na ukweli kuwa ushirikiano na mshikamano miongoni mwa watumishi ndiyo msingi wa mafanikio katika kuwahudumia nchi na watu wake”, alisema Babu.
Aidha alimshauri Mkuu huyo wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa mapato ya Serikali ambayo alisema ndiyo muhimu katika kutekeleza shughuli zote za kimaendeleo hapa nchini.
“Pia nitoe rai kwenu kuhakikisha kuwa mnaweka kipaumbele mikopo inayotolewa kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye kuishi na ulemavu maarufu kama 4-4-2, ambayo alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa maagizo ya kuwa itolewe kwa wakati na bila upendeleo”, alisema.
Aliongeza, “Swala la mikopo ya asilimia 40 kwa Wanawake, asilimia 40 kwa Vijana 40 na asilimia 20 kwa watu wenye kuishi na ulemavu iko wazi na masharti yako wazi na sasa imeboreshwa, kilichoko sasa ni kuhakikisha swala hilo linashughulikiwa ipasavyo ili iwanufaishe walengwa wa mikopo hiyo”.
Kwa upande wake Mkuu huyo wa Wlaya ya Moshi Gogfrey Eliakim Mzava aliahidi kutekeleza majukumu yake kadiri atakavyojaliwa na Mwenyezi Mungu ili kukidhi mahitaji ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amempa dhamana ya kuwahudumia wananchi kwa niaba yake.
“Naomba kumshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, kwa dhamana kubwa aliyonipa; hii ni mara ya pili kunipa dhamana kubwa; kwanza mwaka jana alinipa dhamana ya kuwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na Januari 24, mwaka huu, ameniteua kushika wadhifa wa Mkuu wa Wilaya ya Moshi; ahadi yangu kwake ni kuwa sitamuangusha”, alisema.
Wakiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mwl. Mwajuma Nasombe na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mhandisi Zuberi Kidumo, waliahidi kumpatia ushirikiano Mkuu huyo wa Wilaya mpya ambapo pia wakapata fursa ya kuelezea mafanikio yaliyopo ndani ya Manispaa hiyo.
“Kiongozi mzuri ni yule anaeweza kutafsiri maono ya yule aliyemteuwa; maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuiona Tanzania, ikiwemo wilaya ya Moshi inaendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo, ni matumaini yangu kuwa mkuu wetu wa wilaya tuliempata tutashirikiana naye katika kutafsiri ndoto za kiamedneleo alizonazo Rais Dk. Samia”, alisema.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk.Fredrick Shoo, amemshauri mkuu wa wilaya ya Moshi kwenda kuyaishi yale yote ambayo ameyazungumza katika kiapo chake.
“Uongozi ni utumishi, yale uliyoyatamka hapa tunataka tuyaone katika matendo na utumishi wako wa kila siku. Kiongozi mzuri ni yule ambaye anawatumikia wananchi na haya uliyoyatamka hapa wakati ukiapa tunatarajia kuona ukiyaishi,”alisema Dk. Shoo.
