Wakili wa Serikali atoa wito kwa Wananchi kuchangamkia huduma za ushauri wa Kisheria Bure

MOSHI-KILIMANJARO

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dickson Mbilu ametoa wito kwa wananchi mkoani Kilimanjaro, kuendelea kujitokeza zaidi kupata huduma za ushauri wa kisheria zinazotolewa bure na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hayo aliyasema Januari 26,2025 mjini Moshi  katika standi kuu ya mabasi Moshi,wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa ameridhishwa na mwitikio wa wananchi wanaokuja katika kliniki ya Sheria inayotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano na Kamati ya Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro.

“Mwitikio wa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, kuja kupata msaada wa kisheria ni mzuri, nitumie nafasi hii pia kuwakumbusha kuwa kilele cha kliniki yetu ni kesho Januari 27 mwaka huu, hivyo waendelee kuja kwani tuko tayari kuwahudumia,”alisema Wakili Mbilu.

Kwa upande, wake Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Kamati ya Sheria ya mkoa wa Kilimnajaro Glorian Issangya, ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanya Kliniki ya Sheria bila malipo mkoani hapa kwani imesaidia kutatua changamoto za wananchi wengi waliofika kupata huduma katika kliniki hiyo.

“Niipongeze sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendesha kliniki ya Sheria bila malipo mkoani Kilimanjaro, huduma hii imekuwa na manufaa makubwa sana kwa wananchi wetu kwani kliniki hii imeweza kutatua kero mbalimbali za kisheria zilizokuwa zinawakabili wananchi.” Alisema Glorian Issangya.

Aidha Issangya alieleza kuwa Kamati ya mkoa wa Ushauri wa Kisheria imejipanga kutembelea kwenye maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo ili  kutatua changamoto za kisheria kwa wananchi wa mkoa huo.

“Kamati ya Mkoa ya huduma za Kisheria inajipanga kuwatembelea wananchi katika maeneo yao hususani vijijini ili tuweze kutatua migogoro yao na kuwafanya wananchi wetu wajikite kwenye shughuli za maendeleo.” Alisema Wakili Glorian Issangya.

Naye, David Mongi alisema kuwa kliniki hiyo imekuwa msaada na mkombozi mkubwa kwa wananchi wengi, imeweza kutatua migogoro mbalimbali ndani ya muda mfupi na pia imewasaidia watu ambao wenye kipato cha chini kwani kliniki hiyo imekuwa ikitoa ushauri na msaada wa kisheria bila malipo.

“Mimi nimehudhuria Kliniki hii kwakweli nimefarijika sana na huduma hii, naishuruku Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta jambo hili hapa Kilimanjaro, nimehangaika muda mrefu na jambo langu lakini jopo hili la Mawakili limenihudumia kwa haraka”. Alisema. Mongi.

Kliniki ya Sheria kwa Wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro ilianza Januari 21 Januari 2025 katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi ya Moshi, itafikia kilele chake kwa mkoa wa Kilimanjaro Januari  27, mwaka huu.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.