Serikali mkoa wa
Kilimanjaro imesema, mbio za Kilimanjaro Marathon huchangia kukuza Uchumi wa
mkoa na Taifa kwa ujumla kupitia sekta ya utalii.
Katibu Tawala Mkoa wa
Kilimanjaro Kiseo Nzowa, aliyasema hayo Januari 17,2025 wakati wa uzinduzi wa
msimu wa 23 wa mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International
Marathon, hafla iliyofanyika Hoteli ya
Salinero-Kilimanjaro, iliyoko Moshi, mkoani humo na kuwakutanisha wadau
mbalimbali wa michezo, kabla ya tukio hilo maarufu la kimataifa ambalo
linatarajiwa kufanyika Februari 23, mwaka huu.
Nzowa alisema mbio hizo
ambazo kwa sasa ni maarufu Barani Afrika, zinachangia kukuza uchumi wa Mkoa wa
Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla kupitia sekta ya utalii kutokana na washiriki
wa ngazi zote wanaokuweko mkoani humo kwa
kipindi chote cha mbio hizo.
Alisema serikali itaendelea
kutangaza vivutio vya utalii katika nchi wanazotoka washiriki wa mbio za
Kilimanjaro International Marathon ili kuongeza idadi ya washiriki wengi wa
mbio hizo na hatimaye kuongeza idadi ya watalii nchini.
Alisema serikali imejipanga
kikamilifu kuimarisha ulinzi na usalama kwa washiriki, wadhamini na wadau wote
watakao shiriki katika tukio hilo kubwa linalotarajiwa kufanyika Februari 23,
mwaka huu.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza wadhamini wote wa mbio hizi wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager ambao wanadhamini mbio za kilomita, kampuni ya YAS ambao wanadhamini mbio za kilomita 21 (Yas Half Marathon) pamoja na Benki ya CRDB ambao wanadhamini mbio za kilomita 5”, alisema.
Aidha aliwapongeza wadhamini wengine ambao wanaunga mkono mbio hizo ambao ni pamoja na kampuni ya saruji ya Simba (Simba Cement), Kilimanjaro Water, TotalEnergies, kampuni ya TPC Sugar Ltd, Wasambazaji rasmi GardaWorld, CMC Automobiles, Salinero- Kilimanjaro, Kibo Palace Hotel na Keys Hotel, ambao ushiriki wao umechangia kuendelea kukua kwa mbio hizi”.
Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Khensani Mkhombo, alisema kuwa kampuni hiyo inajivunia kuwa wadhamini wa mbio hizo kwa miaka 23 iliyopita kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuifanya kampuni hiyo kuwa mmoja wa wadhamini wa muda mrefu kwenye tukio moja la kimichezo hapa nchini.
Mkhombo, alisema kuwa udhamini huo ni pamoja na kuboresha ya sekta ya michezo na hivyo kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta ya utalii kwa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kila msimu wa mbio hizi unapowadia.
“Kutokana na mbio hizi kuzidi kupata umaarufu, Mwaka huu, kamati ya maandalizi ya mbio hizi imekuja na mkakati mpya unaolenga kufanya matamasha ya utangulizi ambayo yatakayofanyika siku za mwisho wa wiki kuelekea mbio hizi, amapo matamasha hayo yataanza Ijumaa na kumalizika Jumapili ambayo ndiyo siku ya mbio hizo”, alisema na kuongeza, matamasha haya yanatarajiwa kuboresha biashara mjini Moshi.
Akizungumzia kuhusu zawadi zilizoandaliwa kwa msimu wa 2025, Mkhombo alisema kuwa Kilimanjaro Premium Lager imetenga jumla ya Sh milioni 30, ambapo washidni wa kilomita 42 kwa wanaume na wanawake kila mmoja anatarajiwa kupata zawadi ay shilingi milioni 5.5, ambapo wanariadha wa Kitanzania ambao watashika nafasi ya kwanza katika mbio za kilomita 42 watapata bakshishi ya Sh 550,000 kila mmoja.
Alisema mbali na kukuza sekta ya michezo, mashindano hayo pia yameimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya wadhamini, wandaaji, chama cha riadha nchini RT pamoja na jamii yote kwa ujumla.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Biashara YAS, Isack Nchunda alisema, "Mwaka huu tunaadhimisha na kujivunia kuwa sehemu ya udhamini wa mbio hizi maarufu Barani Afrika kwa muongo wa kumi sasa, kupitia udhamini wetu wa mbio za kilomita 21 maarufu kama Yas Half Marathon, ambapo kitengo hiki kinawaleta washiriki takribani 6,500, wakiwemo wanariadha maarufu Barani Afrika”.
Alisema mwaka huu, wakimbiaji na washiriki wengine wa pembeni kwa maana ya mashabiki wa mbio hizo watarajie kuona mambo mazuri kwenye mbio za kilomita 21 kutokana na uzoefu walionao wadhamini wambio hizo ambao ni Yas, ambapo alitoa rai kwa washiriki wa mbio hizo kujitokeza mapeam kuwahi nafasi zao kabla mbio hizo hazijaanza siku ya tukio hilo.
Kwa upande wake, Meneja Biashara wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, David Peter, alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa mmoja wa washiriki wa Karibu wa mbio hizo maarufu kupitia udhamini wake katika mbio za kilomita 5 za mashindano ya Kilimanjaro Marathon ambayo yanalenga kuboresha afya za watu sambamba na kukuza uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla.
“Kwetu hili ni jukwaa sahihi la kuitangaza benki yetu kwani tunatarajia kuwafikia Watanzania wengi wa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na wale mikoa ya jirani kupitia udhamini wetu wa mbio za Kilomita 5 za Benki ya CRDB,” alisema.
Kwa upande wao Kamati ya waandaaji wa mbio hizo waliwashukuru wadhamini wakuu wa Kilimanjaro Premium Lager na YAS kwa kutenga kitita cha jumla ya shilingi milioni 53 ambazo zitatolewa kama zawadi ya Mbio za kilomita 42 na kilomita 21, pamoja na vitengo vinmgine mbalimbali.
Waandaaji hao pia walisema kuwa tukio hilo mwaka huu, pia linalenga kuchangia asilimia 5 ya kila malipo ya kiingilio kwa ajili ya msaada kwa Shirika la Tumaini la Maisha (TLM), msaada ambao wamesema unalenga kuwahudumia watoto wanaougua ugonjwa wa saratani ili wapate matumaini mapya baada ya kupata matibabu ya ugonjwa huo.
“Pesa zote ambazo zitachangwa kwa ajili ya msaada huo mwaka huu, zitaelekezwa kwenye Kituo cha Matibabu ya saratani wka watoto kilihcoko katika hospitali ya rufaa ya kanda ya KCMC (KCMC ZRH) iliyoko Moshi, mkoani Kilimanjaro”, alisema sehemu ya taarifa ya wandaaji hao.
Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 23, 2025, katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ambapo mbio hizo zimeandaliwa na Kampuni ya Kilimanjaro Marathon na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited, ambapo Kampuni ya Wild Frontiers ndiyo inawajibika na matayarisho yote ya usafiri pamoja na maswala yote ya masoko yanayohusiana na tukio hilo muhimu.
![]() |







