MOSHI-KILIMANJARO
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amezindua rasmi Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro, hafla iliyofanyika Januari 21 mwaka huu katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi Moshi Mkoani humo.
Uzinduzi huo, ulifuatiwa na uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa.
Akizungumza na wakazi wa mkoa huo walioshiriki katika ufunguzi wa Kliniki hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Kilimanjaro na kuja kutoa huduma ya Kliniki bure kwa wananchi wa Kilimanjaro.
“Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi inafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro, huduma hizi zitatolewa katika Viwanja vya Stendi ya vumbi ya Stendi Kuu ya Mabasi mjini Moshi kuanzia Januari 21 hadi 27 Januari 2025.”amesema Babu.
Aidha mkuu huyo wa mkoa , ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kutoa huduma ya kliniki ya bure kwa wananchi wa mkoa huo, hali ambayo inaonesha namna ofisi hiyo ilivyojikita kusogeza huduma karibu na wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Babu ameeleza kuwa Kliniki ya Bure ya Sheria hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya Wanachi dhidi ya Serikali, zitawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria, pia zitawasaidia Mawakili wa Serikali kushirikiana kwa ukaribu na wadau pamoja wananchi katika kutatua masuala ya Kisheria.
"Leo tunakwenda kuanza Kliniki
ya Sheria ni matumaini yangu itawasaidia wananchi wenye matatizo ya kisheria,
kuna timu nzuri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakuwa inatatua
changamoto mbalimbali za wananchi", Amesema Babu.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa
wa Kilimanjaro, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kushiriki kwa wingi katika
Kliniki hiyo ili wapate suluhu ya changamoto mbalimbali za kisheria
zinazowakabili
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tamari Mndeme amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vyema kutoa huduma za Kisheria bure kwa wananchi kupitia Kliniki hiyo.
"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na tuna wataalamu wa kutosha tunaamini kupitia Kliniki hii changamoto mbalimbali za wananchi zitatatuliwa,"amesema Wakili msomi Mndeme.
Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro ni mwendelezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za Kisheria kwa Wananchi.











