Utendaji kazi wa kiwango cha juu wa Serikali
ya Awamu ya Sita katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo umewezesha
Mkutano mkuu wa CCM kumchagua Rais Dk. Samia Suluhu kupeperusha bendera ya
chama hicho tawala kama mgombea urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika baadaye mwaka huu.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
(NEC) Suleiman Mfinanga, ameyasema hayo Januari 30,2025 wakati akiwahutubia
wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro hafla iliyoandaliwa na uongozi wa CCM mkoa wa
Kilimanjaro kuunga mkono azimio la Mkutano Mkuu wa CCM wa kumchagua Dk. Samia
kuwa mgombea wa urais wa chama hicho.
Mfinanga; alisema mafanikio hayo ndio
yamempa nguvu kuchaguliwa kuwa mgombea wa Urais mwaka 2025.
“Ni kweli kwamba mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa ilani ya CCM, hususan chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu, Hassan, yamechangia katika kumjengea umaarufu na kuhamasisha uongozi wake.”alisema Mfinanga.
Alisema miongoni mwa mafanikio ambayo Serikali
ya awamu ya sita imejizatiti katika kuyakeleza ni pamoja na miradi mikubwa ya Kimkakati,
uboresha huduma za kijamii, na usimamia vizuri rasilimali za taifa.
“Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja
na eneo la nchi kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama kwa mijini na vijijini
hali iliyoifanya Serikali kutaka mafanikio hayo yalindwe.”alisema.
Mfinanga ambaye alimwakilishi
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi kwenye hafla hiyo,
iliyofanyika Moshi Mjini, alisema kuwa CCM Mkoa wa Kilimanjaro pia umeunga
mkono uamuzi wa mkutano huo mkuu kumchagua Katibu Mkuu wa CCM Dk. Emanuel Nchimbi
kuwa mgombea mwenza wa Rais Dk. Samia.
“Aidha tunaupongeza uamuzi wa mkutano
mkuu wa kumchagua Dk. Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwani kama
ilivyo kwa Dk. Samia, uongozi wake (Dk. Mwinyi) mahiri umedhihirika kwa
mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi kifupi cha uongozi wake”,
alisema.
Akizungumzia baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana mkoani Kilimanjaro, Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
(NEC) alisema katika sekta ya ujenzi jumla ya Sh bilioni 124.56 zilitumika
kufanikisha miradi mbalimbali katika sekta hiyo.
“Maeneo mengine ni pamoja na sekta ya
Nishati ambayo ilipatiwa jumla ya Sh bilioni 67.2 ambapo wateja wapya 98,940
hadi sasa wameunganishwa kupitia TANESCO na wengine 5,552 wakiwa wameunganishwa
kupitia mradi wa rea”, alisena na kuongeza hayo yote ni katika kutekeleza ilani
ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Aidha Mfinanga aliwapongeza viongozi
wa serikali wa ngazi zote za Mkoa wa Wilaya kwa kusimamia vyema fedha za miradi
zinazotolewa na serikali jambo ambalo alisema linadhihirishwa na utekelezaji
mzuri wa miradi hiyo maeneo mbalimbali mkoani humo.
Akiongea katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, alisema kuwa moja wapo ya mafanikio makubwa ya Serikali ya CCM ni Amani ambayo alisema inaendelea kutamalaki hapa nchini.