Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na Falsafa ambayo imejikita katika masuala ya maridhiano, ustahamilivu mageuzi na kujenga upya taifa, ambayo imeleta mabadiliko chanya hapa nchini.
Waziri Ndumbaro aliyasema hayo jana Mkoani Kilimanjaro, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya MAMA SAMIA LEGAL AID, iliyofanyika katika standi ya zamani ya mabasi mjini Moshi mkoani humo.
Alisema kupitia 4R za Rais Samia, zimeendelea kutamalaki jambo ambalo limewezesha hata kampeni ya Msaada wa Kisheria kuwa na matokeo chanya ya ya falsafa hiyo.
“Falsafa
hii imejikita katika masuala ya Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu
(Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding), 4R hizi zimefanya
nchini kuendelea kuwa na amani,”alisema Waziri Ndumbaro.
Akizungumzia
kampeni hiyo maalum Dk. Ndumbaro alisema kuwa ni matokeo ya maono aliyokuwa
nayo Rais Dk Samia baada ya kubaini ya kuwa watu wengi wana kiu ya haki, jambo
ambalo amesema linadhibitishwa na umati mkubwa wa watu wanaojitokeza kwenda
kupata ushauri wa kisheria kila mahali kampeni hiyo inapofanyika hapa nchini.
“Serikali
ya awamu ya sita iligundua ya kuwa wananchi wengi na wana kiu ya haki na ndipo
Rais Dk Samia kupitia busara zake akaanzisha kampeni hii nchi nzima ili kukidhi
kiu ya haki waliyonayo watu wengi haswa wale ambao hawana uwezo wa kulipia
gharama za wataalam wa kisheria”, alisema.
Dk.
Ndumbaro aliwapaongeza wale wote ambao wamejitokeza kupata huduma zinazotolewa
kupitia kampeni hiyo jambo ambalo alisema limedhihirisha ustaarabu wa
Watanzania wa kutafuta haki kupitia ngazi za kisheria badala ya kuitafuta
kupitia maandamano kama ilivyo kwenye maeneo mengine duniani.
Aidha
Waziri Ndumbaro amewashukuru wasaidizi wa kisheria wa mkoa wa Kilimanjaro kwa
namna ambavyo wanasaidia utoaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa
wahitaji na hivyo kuwezesha wananchi
kupata nafuu na haki inayohitajika kwa mujibu wa sheri.
“Nichukue
fursa hii pia kuwapongeza wanasheria wote na taasisi zote zikiwemo zile za
kibinafsi ambazo zitashiriki katika kutoa huduma wakati wote wa kampeni hii
mkoani Kilimanjaro; huu ni Mkoa wa 17 tangu kuanza kwa kampeni hii, katika
Mikoa 16 iliyopita wanasheria na taasisi mbalimbali wamefanyakazi nzuri, ni
matumaini yetu kuwa kazi nzuri hizo zitaendelezwa hapa mkoani Kilimanjaro
katika muda wote wa kampeni hii kama ulivyopangwa”, alisema.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw Nurdin Babu, alisema kampeni hiyo ni
muhimu kwa wananchi, yenye faida kubwa
na kwamba imekuja wakati muafaka mkoani humo kutokana na ukweli kwamba
watu wengi wana kiu na wengi wao hawana uwezo wa kugharamia huduma za kisheria.
“Sisi
uongozi wa Mkoa tunaahidi kutoa ushirikiano wetu wa dhati katika kipindi chote
cha kampeni hii; tunaahidi ya kuwa tutahakikisha ya kuwa huduma hizi zinafika
hadi ngazi za chini kabisa za kiutawala ikiwemo ngazi ya vijiji ili kila
mwananchi afaidi matunda yanayotokana na maono mazuri ya Rais Samia Suluhu
Hassan na Serikali yake kwa ujumla”, alisema babu.
Naye Mkurugenzi
wa taasisi ya ushauri wa kisheria mkoani Kilimanjaro ya KWIECO Wakili Elizabeth
Minde, alimpongeza Rais Samia kwa kuja na wazo la kambi hiyo ya msaada wa
kisheria.
“Kampeni
hii imeakisi uwezo na maono chanya aliyonayo Rais Samia; itakuwa ya msaada
mkubwa kwa wananchi wengi haswa wakiwemo wale ambao wako maeneo ya vijijini na
ambao kwa sababu moja au nyingine hawakuwa na uwezo wa kulipia gharama kwa
ajili ya kupata huduma za kisheria”, alisema.
Aliongeza
kuwa “Nichukue fursa hii kumpongeza Rais na Serikali ya awamu ya sita kwa
kuanzisha madawati ya msaada wa kisheria katika kila halmashauri jambo ambalo
limewasogezea karibu huduma za kisheria wanachi wa ngazi zote na katika wilaya
zote hapa nchini”.
Awali
akiongeza Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface
Mwabukusi, ameisistiza jamii kuto puuza swala la kuandika wosia ili kuepusha
changamoto zinazo jitokeza katika ugawaji mali.
“Kuna
faida nyingi za kuandika wosia kwani mali zitagawanywa kulingana na maelekezo
ambayo yaliachwa na marehemu na hivyo kuepusha ugomvi na mitafaruku mbalimbali
ambayo ingetokea kutoka katika familia na ukoo mzima.”
“Changamoto kubwa zinazowagusa wananchi ziko kwenye ardhi na mirathi, ardhi inachangiwa na utafsiri mbaya wa sheria na upande wa mirathi ni kutokana na watu kutokupenda kuandika wosio,”alisema.