DODOMA
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Miswada Miwili ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2024, Januari 29, 2025 katika kikao cha pili cha Mkutano wa kumi nane wa Bunge hilo.
Miswada iliyopitishwa leo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mbalimbali (Na.3) wa Mwaka 2024 (The written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 3) Bill 2024, na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2024 (The written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 4) Bill 2024No. 3) Bill 2024.
Akizungumza wakati
wa kuwasilisha Miswada hiyo, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari amesema kuwa Miswada hiyo inakusudia kufanya marekebisho
katika jumla ya Sheria kumi na mbili.
"Malengo ya
marekebisho haya ni kuboresha utekelezaji wa masharti ya sheria husika na
kuzifanya sheria hizi ziendane na wakati na kuleta tija kwa
wananchi". Amesema Mwanasheria Mkuu
wa Serikali
Aidha, Mwanasheria
Mkuu amezitaja Sheria zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Mawakili Sura ya
341, Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu Sura ya 3, Sheria ya
Huduma za Jamii Sura ya 291, Sheria ya Shirika la Soko la Kariakoo Sura ya
132, Sheria ya Madini Sura ya 123 na Sheria ya Utumishi
wa Umma Sura ya 298.
Mhe. Johari ameendelea kuzitaja Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji wa
Fedha Haramu Sura ya 423, Sheria ya Vyama vya Ushirika Sura ya 211, Sheria ya
Tasnia ya Pamba Sura ya 201, Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji wa Kiuchumi Sura ya
386, Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji Sura ya 435, Sheria ya Ukaguzi wa Umma Sura
ya 418.
Katika hatua
nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema
marekebisho hayo yatasaidia kutatua changamoto na mapungufu mbalimbali yaliyokuwepo
katika sheria hizo.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu
ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Joseph Mhagama amefurahishwa na hatua za
Bunge kupitisha Miswada hiyo ambayo inaenda kuleta maboresho katika utekelezaji
wa Sheria zilizorekebishwa hivyo kupelekea mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii
kwa watanzania.
"Nalipongeza Bunge kwa kupitisha Miswada hii miwili ambayo inakwenda kuboresha na kuleta tija katika Sekta mbalimbali". Amesema Waziri Mhagama.
Baada ya Miswada
hiyo kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapelekwa kwa Rais
ili iweze kusainiwa na kuwa Sheria kamili.