Jinsi Kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilivyoibua ukatili aliofanyiwa mtoto wa miaka 5 na Bibi yake
Unyama huo umepelekea mtoto huyo kukatwa mguu.
KISANGARA-MWANGA
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya
Mama Samia (MSLAC), imeibua makubwa mkoani Kilimanjaro baada ya kubainika kuna
mtoto ambaye amepata ukilema baada ya kufanyiwa ukatili na Bibi yake.
Akizungumzia kisa hicho jana, wakati
akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kisangara iliyoko wilaya ya
Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Afisa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji Halmashauri
ya Mwanga Alexs Kameo, alisema mtoto huyo alipata kilema hicho baada ya kupigwa
na Bibi yake huyo.
“Mtoto huyo wa miaka mitano
alipigwa na Bibi yake ikiwa ni adhabu kwa kile kilichodaiwa ya kuwa alifanya
kosa jambo lilipelekea kupata jeraha kubwa juu ya paja la goti”, alisema.
“Hata hivyo Bibi yake huyo
alisita kumpeleka hospitali kutibiwa jeraha hilo kwa kuhofia kuwa ikigundulika
mtoto huyo amelipata jereha kwa kumwadhibu atachukuliwa hatua za kisheria
ikiwemo kufungwa jela”, alisema.
Kameo, aliendelea kusema kutokana
na hofu hiyo, Bibi huyo aliamua kumfungia mtoto huyo ndani kwa muda mrefu hadi
kidonda alichopata mtoto huyo kilioza na kuanza kutoa harufu.
“Kila Bibi alipokuwa akiulizwa na
majirani kuhusiana na mtoto huyo yuko wapi, alikuwa akisema amesafiri kwenda
kwa ndugu wengine; hata hivyo siku moja wageni waliofika nyumbani kwa Bibi huyo
wakasikia harufu kali na kuhoji inatokea wapi na ndipo baada ya kufanywa
uchunguzi wa kina ikagundulika mtoto huyo alikuwa amefungiwa ndani”, alisema.
Wageni hao waliamua kwenda kutoa
taarifa kwa Mwenyekiti wa kitongoji na ndipo alipokuja na kufungua mlango wa
chumba alichokuwa amefungiwa huyo mtoto kna kukutwa akiwa humo ndani akiugulia.
“Mtoto huyo alipelekwa hospitali
ya KCMC, lakini ikasemekana mguu wa mtoto huyo tayari umekwisha kuoza na hivyo
ikabidi ukatwe”, alisema.
Hata hivyo kila mtoto huyo
alipokuwa akiulizwa ni nini kilichompata alikuwa akisema ya kuwa ameumizwa na mtoto
mwenzake wakati wakicheza.
“Baada ya kupata huduma KCMC mtoto
huyo alipelekwa kwenye kituo cha malezi ya watoto na pale walifika Wanasaikolojia na kuzungumza na mtoto
huyo ili kutaka kupata ukweli wa kile kilichomsababishia mguu wake kukatwa.
Katika simulizi yake hiyo, Kameo alisema
mtoto huyo baada ya kuhojiwa kwa kina na Wanasaikolojia akakiri ya kuwa Bibi
yake ndiye alimuadhibu na alipopata jereha hilo alimwambia akisema kuwa
alimpiga tamuua ndipo akaogopa kusema”, alisema.
“Tumeona umuhimu wa kwenda kwenye shule hiyo ili kutoa elimu kuhusiana na Msaada wa Kisheria, lakini pia tumewafundisha elimu kuhusiana na sheria ya mtoto ili waweze kujua kwamba wana wajibu gani na haki gani kulingana na miongozo ya kisheria,”alisema.
Alisema aliamua kuwaelezea kisa hicho
ili kuwajengea uwezo kwamba wanao ujasiri wanaweza kujikwamua kutoka kwenye
mnyororo wa kufungwa, kushindwa kutoa taarifa, au kwa kuhisi kwamba wakitoa
taarifa wazazi wao watakuwa na changamoto za kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Mtoto huyu ni yatima baada ya
kupoteza wazazi wake wote wawili na kwa mujibu wake yeye mweyenyewe anampenda
Bibi yake na anamtegemea hivyo akaogopa kusema yaliyompata kwa kuhofia bibi
yake atafungwa na atabaki na nani”, alisema.
Alisema baada ya shauri hilo kupelekwa polisi na hatimae kufikishwa mahakamani lakini likaondolewa mahakamani hapo baada ya kukosa ushahidi.
“Huu ni mfano mmoja tu wa mambo
mengi ambayo watoto wengi na hata watu wazima wanafanyiwa ukatili wa aina
mbalimbali lakini wanashindwa kuripoti vitendo wanavyofanyiwa kwa ajili ya vitisho
wanavyopata kutoka kwa waliowafanyia vitendo vya ukatili”, alisema.
Kwa upande wake Afisa Wahudumu
Msaada wa Kisheria Innocent Muro, alisema Rais Samia baada ya kuona changamoto
hizo aliona kuna haja ya kuwa na kitengo cha Msaada wa Kisheria kwa wananchi
ambao wanashindwa kukidhi gharama za kuendeshea mashtaka yao pindi yanapokuwa
katika mahakama.
“Baadhi ya watu ambao wanakumbwa
na changamoto za Huduma ya Msaada wa Kisheria ni watu wenye vipato vya chini, wako
watu wenye uwezo wa kipato cha kifedha wanatumia kama shehemu ya kuwakandamiza
watu wenye uchumi mdogo kuwanyima haki zao.”alisema.
Pia Muro alielezea Kampeni hiyo yenye maudhui ya kusaidia wananchi ina mambo 10 na itapita kila eneo la Tanzania Bara na Visiwani, ambapo kwa Wilaya ya Mwanga Kampeni hiyo wamevifikia vijiji vitatu vya Mangara, Mbambua na Kisangara vilivyoko Kata ya Lembeni, pamoja na shule ya sekondari Kisangara na shule ya msingi Kisangara.