Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai, amewataka
vijana wanaotokana na (UVCCM) na Wana CCM kwa ujumla wasiogope kuzitangaza kazi
ambazo zimefanywa wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi chote tangu
alipoingia madarakani Machi 19, mwaka 2021.
Swai; aliyasema hayo Februari 1, 2025 wakati aliposhiriki zoezi la usafi kwenye zahanati ya Shirimatunda iliyoko Manispaa ya Moshi, ikiwa ni Maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa CCM, iliyoenda sambamba na kuunga mkono maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kwa kumchagua Rais Samia kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwaka huu.
Alisema
tangu kuingia mardarakani Rais Samia, Watanzania wameshuhudia mageuzi makubwa
ya kiuchumi katika nyanja mbalimbali, ikiwemo ile ya afya, elimu, maji, kilimo
na barabara.
Akizungumzia
sekta ya afya alisema imekuwa kichocheo kikubwa cha kuwasaidia wananchi wanaoishi
maeneo ya mbali serikali imejenga zahanati kila kata pamoja na kununua vifaa
tiba ili kuwasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao.
“Serikali imeendelea na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini, ambapo miundombinu hiyo inahusisha hospitali za rufaa za Kanda, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati,”alisema Swai.
Kuhusu sekta ya elimu Swai alisema, serikali imeendelea kujenga miundombinu ya elimu, kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora na yenye staha.
Miradi mingine ambayo Swai aliielezea ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa kufua umemev wa maji wa Mwl. Julius Nyerere, mradi wa ujenzi wa Bomba la mafuta Ghafi , ujenzi wa barabara na madaraja pamoja na miradi ya Kimkakati ukiwemo mradi wa Reli ya Kisasa kwa kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway-SGR).
Kwa upande wake Katibu wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro Ahmady Kibamba, aliwashukuru uongozi wa UVCCM Moshi Mjini kwa kuweza kuratibu shughuli hiyo na kutimiza maelekezo ya CCM, ambayo walipewa ya kuadhimisha miaka 48 ya CCM kwa kila Wilaya.
Aidha
Katibu huyo aliwataka vijana wenye nguvu, uwezo nia na uthubutu, wenye sifa za
maadili ya kuwa viongozi wajitokeze kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pale zinapotangazwa na chama.
“Nawaomba tusiwe vijana wa Iyena Iyena tu, lazima tuwe vijana wenye mipango, ukitoka kuwa
Katibu wa Kata wa vijana, unatakiwa uende hatua nyingine ya kuwatumikia vijana
na watanzania kwa ujumla,”alisema Kibamba.
Aliongeza
kuwa “Kura zisipotosha utajipanga kwa awamu nyingine, kwani ziko fursa nyingi,
kuna nafasi za UWT wilaya na mkoa akina dada mnao uwezo wa kwenda huko, tunataka
kuwa na kundi kubwa la vijana wenye nguvu ya kukisaidia chama na serikali,
sipendi sana kuona vijana wakikimbizana tu bila kuwa na mipango na malengo,”alisistiza.
“Kata ya Shirimatunda tulipokea Sh bilioni 1.3 ambazo zimewezesha kujenga jengo la mama na mtoto, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa Nje, maabara, chumba upasuaji, chumba cha kufulia sambamba na ukarabati wa majengo ya zamani ya zahanati ya Shirimatunda,”alisema.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi Sadath Ndibalema, alisema Uongozi wa UVCCM wilaya hiyo, inaunga mkono uamuzi wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)wa kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama heshima ya kuenzi uongozi wa matokeo yake.




















