MOSHI-KILIMANJARO.
Serikali mkoa wa Kilimanjaro, imewataka
viongozi na watendaji wa mamlaka za serikali za mitaa, kutekeleza majukumu yao
kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ili kulinda misingi ya utawala bora.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu,
aliyasema hayo Februari 3,2025, wakati akifungua mafunzo kwa wajumbe wa kamati
ya usalama ya Mkoa, wajumbe wa kamati ya usalama ya wilaya ya Moshi, watendaji
wa kata na wakuu wa idara wa wilaya hiyo, wakati wa mafunzo kuhusu elimu ya
Uraia na Utawala Bora yaliyofanyika
ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa, Katibu
Tawala wa mkoa huo Kiseo Nzowa, aliwataka viongozi hao kuhakikisha kwamba pindi
wanapotekeleza majukumu yao ya kazi, wazingatie haki za binadamu, utawala bora,
maadili na miiko ya uongozi.
“Napenda kuipongeza Wizara ya Katiba na
Sheria kwa kubuni na kuendesha mafunzo haya muhimu ya masuala ya Uraia na
Utawala Bora kwa Kamati za Usalama na Watendaji wa halmashauri .”alisema Kiseo.
Alisema
mkoa wa Kilimanjaro, unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo utekelezaji
wa haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora huku akizitaja
changamoto hizo kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa misingi ya haki za binadamu
miongoni mwa jamii.
“Mafunzo haya yanafanyika kwa wakati muafaka kwa kuwa katika mkoa wetu wa Kilimanjaro zipo changamoto kadhaa katika utekelezaji wa haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora, baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na uelewa mdogo wa misingi ya haki za binadamu miongoni mwa jamii, mila na destuli kandamizi, vitendo vya ukatili wa kijinsia na vitendo vya ubakaji,”alisema.
Awali akizungumza Mkurugenzi wa Idara Katiba
na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Jane Lyimo, alisema Wizara
ya Katiba na Sheria imeendelea kuwa
kinara kwa kutekeleza kwa vitendo na kuiishi falsafa ya 4Rs ya Rais Dk. Samia
Suluhu Hassan kwa vitendo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Serikali
ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada za
kuendelea kuwapambania wananchi wake kupitia falsafa yake ya 4Rs na sisi kama Wizara
ya Katiba na Sheria ni moja ya vinara wa utekelezaji wa falsafa hizi,”alisema
Lyimo.
Akiwasilisha mada ya Ulinzi na Usalama wa Nchi kwa washiriki wa mafunzo hayo Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Wakili wa Serikali Nicholaus Mhagama, aliwasihi watendaji kata, kuacha kung’ang’ania kutatua migogoro ambayo hawajaisomea, huku akitolea mfano wa migogoro ya ndoa ambayo walikuwa wakiitatua kwa kutumia uzoefu badala ya elimu maalum.
Kwa upande wake Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora (THBUB) Juliana Raurent, alisema ukiukwaji wa haki za binadamu unachangia
umasikini mkubwa katika jamii.
“Suala la umasikini ni changamoto kubwa amabayo
inafanya haki za binadamu ziweze kuvunjwa pasipo sisi wenyewe kuzitambua , kwa
umasikini huo anajikuta anadhalilika utu wake, lakini pia mila na desturi
tulizonazo ni changamoto kubwa kwa jamii yetu.”








