Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaendelea kuzingatia masilahi ya nchi kwenye Mikataba mbalimbali ambayo nchi inakusudia kuingia kwakua Kikatiba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo yenye dhamana ya upekuzi na tathimini ya mikataba inayoingiwa na Serikali na taasisi zake.
Dk. Samia aliyasema hayo Februari 3, 2025, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Sheria Nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini, Dodoma.
Aidha, Rais Samia aliwataka Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kuzingatia weledi wakati wa kufanya upekuzi na tathimini ya mikataba mbalimbali ambayo Serikali inayokusudia kuingia.
“Katika kuhakikisha masilahi ya nchi yetu yanaendelea kuzingatiwa kwenye mikataba itakayoingiwa ni lazima Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wawe na uwezo na ubobevu kwenye masharti ya Kimikataba yanayogusa sekta za kiuchumi na uwezo wa kusimamia mikataba hiyo”. alisema Dk. Samia.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Hamza Johari, akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria
nchini alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeendelea kufanya upekuzi
na tathimini kwenye mikataba mbalimbali ambapo kwa kipindi cha kuanzia Julai
hadi Disemba 2024 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikuwa imepekua
Mikataba 1,799 na Hati za Makubaliano 352.
“Kati ya Julai hadi Disemba, 2024 jumla ya Mikataba ya Kitaifa, Kikanda 10 na Kimataifa 1,799 na Hati za Makubaliano (Memoranda of Understanding) 352 zilifanyiwa upekuzi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.” alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine Johari alisema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuwahimiza Mawakili wa Serikali na Wanasheria wote walio katika utumishi wa umma kujiendeleza na kushiriki mafunzo ya fani mbalimbali na sio fani ya Sheria tu ili waweze kufanya upekuzi wa Mikataba na Hati za Makubaliano kwa ufanisi na ufasaha.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake anaoutoa katika kuimarisha miundombinu ya Mahakama nchini.
“Nichukue nafasi hii kukushukuru Rais Samia na Serikali unayoiongoza kwa namna ambavyo umewezesha kuboreshwa kwa miundombinu mbalimbali ndani ya mahakama, tunakushuru sana kwa uwezeshaji wako mpaka sasa Mahakama tunaweza kutanua wigo wa kutoa haki kwa wananchi”. alisema Jaji Mkuu wa Tanzania.
Aidha Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Juma aliwakumbusha watendaji mbalimbali wa mahakama kufanya maboresho katika utendaji wao na kubadilika kifkira ili waweze kutoa huduma zenye ubora kwa wananchi.
“Kila baada ya miaka mitatu tuna kawaida ya kufanya utafiti kutumia Taasisi ya nje ili kuona kama wananchi wanaridhika na huduma zetu, na kutuwezesha kuboresha zaidi huduma tunazozitoa.” alisema Prof. Ibrahim Juma.









