Kamati ya Ushauri wa Kisheria mkoa wa Kilimanjaro yatakiwa kwenda maeneo ya vijijini kutatua changamoto zinazowakabili wananchi

MOSHI-KILIMANJARO

Kamati ya Kisheria iliyoko mkoa wa Kilimanjaro, imetakiwa kuweka utaratibu wa kwenda kwenye maeneo ya vijijini zaidi kwa lengo la kutatua kero mbalimbali za kisheria zinazo wakabili wananchi katika maeneo yao.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, aliyasema hayo Januari 21,2025 wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa.

Babu alisema uweko wa migogoro mingi inawafanya wasifanye kazi za serikali, wanazotakiwa kwenda kuzisimamia jambo ambalo linawafanya kushindwa kusimamia miradi  ya maendeleo na hivyo kubakia wakisuluhisha  migororo.

“Migogoro mingi inatufanya tusifanye kazi za serikali, tunatakiwa tukasimamie shughuli za maendeleo, kwani Rais Samia Suluhu Hassan, ameleta fedha nyingi za maendeleo kwenye mkoa wetu, kwa sasa sisi tunatakiwa kwenda kuisimamia miradi hiyo ikiwemo ya ujenzi wa madarasa, vituo vya afya, barabara na maji lakini tunaacha na kwenda kusuluhisha migororo’,alisema RC Babu.

Akizungumzia kliniki ya Bure ya Sheria, Mkuu huyo wa mkoa alisema itasaidia kupunguza mashauri dhidi ya serikali na hivyo kuchochea shughuli za maendeleo, uwekezaji jambo ambalo litakwenda kuongeza ushirikiano mkubwa kwa wananchi.

“Changamoto kubwa iliyopo katika mkoa wetu ni masuala ya ardhi, mirathi, ukatili wa kijinsia, ukienda kwenye baraza la ardhi la mkoa unawakuta watu saa kumi na moja alfajiri tayari wameshafika kwa ajili kusikilizwa mashauri yao,”alisema.

Aliongeza kuwa kutokana na uwepo wa migogoro ya ardhi katika jami,  ameziagiza Kamati hizo kukaa angalu mara moja kwa robo mwaka kwa ajili ya kutekeleza majukumu yake ya kusikiliza malalamiko ya kisheria na kutoa elimu kwa umma.

Awali akimkaribisha mkuu wa mkoa, Kaimu mkuu wa Wilaya Moshi mshikizi Mwanahamisi Munkunda, alisema wananchi wakipatiwa elimu juu ya uelewa wa kisheria itasaidia kupunguza migororo ya ardhi ambayo ndio changamoto kubwa kwao.

Alisema Ofisi za Wakuu wa Wilaya na ofisi ya mkuu wa mkoa zimekuwa zikipokea malalamiko mengi yanayohusu ardhi, mirathi na uelewa mdogo wa wapi wapeleke jambo hilo.

“Niipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja na mkakati huu wa kuwasaidia viongozi waliopewa dhamana na Rais Samia, kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.”alisema DC Munkunda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa wa Kisheria mkoa wa Kilimanjaro Tamari Mndeme, alisema kamati hiyo itakwenda kuhakikisha inapunguza  migogoro hiyo hususan ili ya masuala ya kisheria.

“Kamati za Ushauri wa Kisheria za Mikoa na Wilaya zimeanzishwa kwa mujibu wa mwongozo wa huduma za ushauri wa kisheria katika mikoa na wilaya, ambayo imetungwa chini ya kifungu cha 21 cha sheria ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  sura ya 268.”

Kikao hicho cha wadau wa Kliniki ya Kisheria kimewakutanisha pia wadau wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambao ndio waratibu wakuu wa Kliniki ya Kisheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.