SAME-KILIMANJARO
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chana, amewapongeza Wakuu
wa Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, kwa ubunifu wao katika kutangaza vivutio vya
utalii, vilivyopo Kanda ya Kaskazini.
Hayo yalijiri wakati wa kufungua Msimu wa Pili wa
Tamasha la Utalii Same, lililofanyika katika viwanja vya Stendi Kuu ya
mabasi Wilayani humo, ambapo Waziri Chana alitaja juhudi za viongozi hao,
katika kukuza sekta ya utalii kama mfano mzuri wa ushirikiano na uongozi bora.
Amesema kuwa mikakati ya kipekee ya kuutangaza maeneo mbalimbali
ya kiutalii katika mikoa hiyo, inachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi na
kuongeza mapato kwa taifa.
‘Naomba nimpongeze sana mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda, kwa
namna ambavyo amekuwa mbunifu wa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo
katika mikoa wake, na kuufanya utalii kuwa ni miongoni mwa vipaumbele
katika mkoa huo, unapofika Jijini Arusha bustani zilizopo kwenye mizunguko ya
barabara (roundabout) zina vivutio vya utalii vinavyotangaza vivutio vya utalii
vinavyopatikana ndani ya mkoa huo.”amesema Waziri Chana.
Pia Waziri Chana amempongeza Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin
Babu, kwa kuja na tamasha mahususi kwa ajili ya kuenzi utamaduni wa asili,
ambalo linakwenda sambamba na kuvitangaza vyakula vya kiasili, vikundi vya
nngoma za asili, mavazi na michezo mbalimbali.
Aidha Waziri Chana, alizitaka halmasahuri zote nchini, kuanzisha
matamasha ya utalii na uhifadhi huku akielekeza suala la kulinda wananchi dhidi
ya wanyamapori wakali na waharibifu iwe ajenda ya kudumu.
Vile vile Waziri huyo, ameielekeza halmashauri ya Wilaya ya Same, kutenga bajeti ya kila mwaka ili kusaidia kuandaa tamasha hilo na sio kuuachia uongozi wailaya pamoja na wadau wachache kuandaa tamasha hilo.
“Wizara yangu, inataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali walioko kwenye kila wilaya na mikoa, ili kufanya matamasha kama lililofanyika Wilayani Same, liweze kukuza na kuendeleza utamaduni wa makabila mbalimbali, kukuza utalii wa kiutamaduni na hatimaye kuongeza ajira na vipato kwa vijana.”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni, amesema tamasha hilo, limeonesha mafanikio makubwa ambapo wawekezaji watatu, wamejitokeza kuanza ujenzi wa hoteli kubwa za kisasa ,ambapo hoteli moja inajengwa mbele ya lango la hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na hoteli mbili zikijengwa hifadhi ya mazingira asilia ya Chome maarufu msitu wa Shengena.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, amesema Tamasha la Utalii Same, limekuwa na matoke chanya ya kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyoko wilaya humo, ambapo uchumi wa wananchi, unaotokana na utalii umeongezeka kupitia watalii wanaokuja kutembelea maeneo yenye vivutio vilivyoko wilayani humo.