Mkuu wa Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro Kasilda Jeremiah Mgeni, akiwahutubia wananchi wa wilaya hiyo, wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Same Utalii Festival Two, Desemba 20,2024. linalofanyika viwanja vya Standi kuu ya mabasi mjini humo.
SAME-KILIMANJARO.
Mkuu wa Wilaya ya Same,
Kasilda Mgeni, amesema vivutio vya utalii vilivyopo wilayani humo,
vimewanufaisha wakazi wa wilaya hiyo.
Hayo ameyasema Desemba
20,2024, wakati akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo waliojitokeza kushiriki maonesho
ya Tamasha la Utalii Same Festival, linalofanyika viwanja vya standi kuu ya
mabasi mjini Same.
“Wageni wanapoingia
Same, wanatumia usafiri, wanakula vyakulana kulala ambapo huchangia pato,
lakini pia wajasiriamali wanapata fursa ya kuuza bidhaa zao,”amesema DC Mgeni.
Amesema sekta ya utalii,
imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na kutoa fursa za
ajira kwa vijana.”amesema.
Aidha amesema Serikali ya
awamu ya sita, imeendelea kufanya juhudi
za kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inapata mafanikio makubwa na kuvutia
wawekezaji wengi hapa nchini, huku akitolea mfano wa filamu ya Royal Tour.”
Akizungumzia umuhimu wa Tamasha
hilo Festival, mkuu huyo wa wilaya amesema, wajasiriamali wadogo wameweza
kunufaika na fursa mbalimbali, ikiwemo
kuuza bidhaa zao na kujiongezea kipato na hivyo kuchangia pato la taifa.
Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emmanuel Moirana, amesema uwepo wa mradi wa Mbwa mwitu na Faru ndani ya hifadhi hiyo umefanya idadi ya wageni kuongezeka kutembelea hifadhi hiyo.
Amesema kuwepo kwa mradi
wa Mbwa mwitu na Faru idadi ya
watalii, imekuwa ikiongezeka, jambo ambalo limeonyesha mwamko kwa wananchi
kutembelea vivutio hivyo.
“Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, ilichanguliwa
kama hifadhi ya uzalishaji wa Mbwa mwitu, kutokana na eneo hilo kushabihiana na
mazingira wanayoishi mbwa hao, mradi huu
ulianza ukiwa na mbwa mwitu 25 ila kwa sasa wameongezeka na kufikia zaidi ya
300,”amesema.
Aidha amezitaja faida zinazotokana na Mbwa mwitu hao kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii hususan kwa wageni ambao wengi wamekuwa wakitembelea hifadhi hiyo kutokana na uwepo wa kivutio hicho cha mbwa mwitu.