Tamasha la Utalii Same Festival limechangia kuongezeka kwa uchumi

SAME-KILIMANJARO

Tamasha la kila mwaka la “Utalii Same Festival” limechangia kukua kwa uchumi kwa wakazi wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, kutokana na idadi kubwa ya watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii, ikiwemo Hifadhi ya Taifa Mkomazi, msitu wa Shengena pamoja na mlima Kidende, vilivyopo wilayani humo.

Hayo yameelezwa Desemba 20,2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Kiseo Yusufu Nzowa, alipotembelea mabanda ya maonesho ya Tamasha la Utalii Same awamu ya pili, yanayofanyika katika eneo la kituo kikuu cha mabasi kilichoko Same mjini, wilayani humo.

“Ongezeko la watalii wanaotembelea wilayani Same, umechangia mapato ya wilaya kuongezeka, lakini pia na yale ya  mtu mmoja mmoja, kutokana na watalii wengi kuhitaji huduma mbalimbali zikiwemo za chakula, malazi pamoja na usafiri”, amesema Nzowa.

Ameongeza, “Haya yote ni matokeo ya Tamasha hili ambalo limekuwa likiwavutia watu kila mwaka kuja kutembelea maeneo mbalimbali pamoja na vivutio vya utalii ambavyo ni pamoja na mali ya kale yaliyoko wilayani Same”.

Katibu Tawala huyo, amevitaja vivutio hivyo kuwa ni pamoja na jengo la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Pare (KKKT-DP) lililoko kijiji cha Manka, kata ya Mshewa ambalo lilijengwa mwaka wa 1908, ambalo amesema kuwa liko kwenye mchakato wa kuingizwa kwenye orodha ya mali za kale.

Nzowa ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu katika shughuli hiyo, ametoa wito kwa wawekezaji kuanza mchakato wa kuwekeza katika maeneo ambayo kuna vivutio vya utalii wilayani humo.

“Tamasha hili limewajengea wananchi uelewa wa swala zima la utalii, hili litachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa utalii wa ndani hivyo kuwekeza mapema kutachangia ongezeko hilo, maana wananchi wanaotarajiwa kutembelea vivutio wilayani Same watakuwa na uhakika wa huduma mbalimbali”, amesema.

Amesema kuwa Tamasha la Utalii Same Festival pia limewajengea wananchi uelewa wa dhana ya kutunza mazingira na raslimali zingine za Taifa kutokana na elimu ambazo hutolewa kipindi cha tamasha hilo kila mwaka.

Aidha Nzowa,  amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kushiriki kivitendo kuutangaza utalii wa Tanzania kupitia filamu ya Royal Tour Tanzania.

“Ushiriki wa Rais kivitendo umehamasiha wawekezaji katika sekta ya utalii hapa nchini nao kuibuka na mbinu mbalimbali za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake ikiwemo kupitia matamasha mbalimali ikiwemo hili la Utalii Same Festival”, amesema Nzowa.

Ameongeza, “Tayari watu wamehamasika, huku akitoa rai kwa wandaaji wa Tamasha hilo, ambalo linafanyika kwa mara ya pili mwaka huu, kuhakikisha linaendelea kukua ili kuongeza idadi ya watalii kuja  kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii mkoani Kilimanjaro, hususani katika wilaya zingine za mkoa huu, hivyo nitoe rai kwa wandaaji wa Utalii Same Festival kuhakikisha tamasha hili linafanyika kila mwaka ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea mkoa wa Kilimanjaro”.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni, amesema lengo Tamasha hilo limelenga kuunga mkono juhudi za serikali zinazoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan za kukuza sekta ya utalii hapa nchini, sambamba na kukzua uchumi wa wananchi wa wilaya ya Same.

“Ndani ya miaka hii miwili, tamasha hili limechangia kunufaisha wananchi ambao hutangaza bidhaa zao kupitia maonyesho na hivyo kupanua wigo wao wa kupata wateja jambo ambalo limewaongezea mapato”, amesema DC Mgeni.

Amesema, kupitia Tamasha hilo, wananchi wamepata fursa za ajira, ikiwemo ile ya kuwatembeza watalii kwenye vivutio mbalimbali na pia tayari uwekezaji umeanza kufanyika ukiwemo wa ujenzi wa hoteli za kitalii zenye hadhi ya nyota tatu unaoendelea wilayani hapa.

Naye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emmanuel Moirana, amesema uwepo wa miradi ya Faru na mwitu katika hifadhi hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watalii wanaotembelea hifadhi hiyo.

Aidha ametao wito wananchi kujenga tabia ya kutembelea vivutio vya utalii vivivyoko wilayani Same sambamba na kulinda vivutio vya utalii na rasilimali zingine za Taifa ambazo amesema ni muhimu katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.