Kibong’oto yapokea Sh bl 2 za ujenzi wa jengo la utawala, radiolojia


SIHA-KILIMANJARO.

Serikali ya Tanzania, imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto (KIDH) iliyoko Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, ambapo imetoa kiasi cha Sh bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Utawala.

Mkurugenzi wa Kibong’oto Dk. Leonard Subi, ameyasema hayo Desemba 19, 2024 wakati wa hafla ya kuwazawadia wafanyakazi wa hospitali hiyo mchele kilo 10 kila mtumishi kwa ajili ya Sikukuu ya Krismasi na ile ya Mwaka Mpya wa 2025, iliyofanyika hospitalini hapo.

“Fedha hizi tulizozipokea jana ni muendelezo wa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya taasisi hii ambapo ndani ya miaka mitatu iliyopita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, tayari serikali imeshatoa zaidi ya 35 kwa ajili miradi ya maendeleo”, amesema Dk. Subi.

Amesema fedha hizo zimetumika kujenga Maabara ya Afya ya Jamii katika ukanda wa Afrika Mashariki na ya Kati na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maboresho katika sekta ya afya hapa nchini ambayo sasa yanaonekana kupitia kazi nzuri inayofanywa na Kibong’oto.

"Mchango huu mkubwa wa serikali umechangia KIDH kupata Ithibati ya Kimataifa ya Vipimo vyake vya Maabara 52 vinavyotambuliwa na kutolewa na Huduma ya Ithibati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCAS)", amesema.”Dk. Subi.

Akizungumzia Sh bilioni mbili zilizotolewa na serikali Dk. Subi amesema zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala ambalo linatarajiwa kugharimu Sh bilioni 1.5, huku kiasi cha Sh milioni 482 zinatarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi wa jengo la radiolojia liliko hospitalini hapo.

Akizungumzia hafla hiyo, Dk. Subi amesema, imelenga kuwakutanisha watumishi wa sekta ya afya, wafanyakazi wa taasisi pamoja na uongozi wa juu wa taasisi hiyo wakati wa kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka, ili kukumbushana yale yote waliyoyafanya kwa mwaka mzima.

"Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, tumekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyakazi wetu kila mwaka, ili kutafakari kazi tulizozifanya kwa mwaka mzima pia kuzawadiana ikiwemo vyakula ili kila mfanyakazi awe na wakati mzuri na familia yake kipindi chote cha Sikukuu."amesema.

Wakiongea kwa niaba ya wafanyakazi wenzao, kwenye hafla hiyo Lightness Munisi, Sarah Senkoro na Saidi Salum, wameushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa zawadi hizo ambapo wamesema uamuzi wa uongozi wa hospitali hiyo kuwazawdia kipindi hiki cha Sikukuu utawapa ari ya kuendelea kuwahudumia watu wanaofika hospitalini hapo kupata huduma mbalimbali.

 


 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.