SAME-KILIMANJARO.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Methusela Ntonda, amesema kwamba ukuaji wa
matamasha ya utamaduni utachochea maendeleo ya sekta ya Utalii, na hivyo
kuvutia watalii wengi kutembelea vivutio mbalimbali nchini.
Akitoa salamu za Waziri wa Wizara
hiyo kwenye ufunguzi wa Tamasha la Utalii Same, Ntonda amesema kuwa tamasha
hilo litachangia kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi na pia litasaidia
kutangaza na kuhifadhi utamaduni, mila na desturi za watu wa wilaya ya Same.
Ntonda amesema ukuaji wa
matamasha ya utalii, yatasaidia kuimarisha sekta ya utalii kwa manufaa ya taifa,
jambo ambalo litasaidia kukuza utamaduni, mila na desturi za taifa kuweza
kudumishwa zaidi.
“Ukuaji wa tamasha hili
utachochea kuvutia utalii wa taifa na pia kuendelea kutangaza utamaduni, mila
na desturi za watu wa same, na hivyo kuweka utamaduni wa taifa kuwa endelevu na
kuimarisha masula ya utalii,”amesema Ntonda.
Pia amempongeza mkuu wa wilaya ya Same kwa kuja na wazo la kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika wilaya hiyo, na kwamba kama Wizara itaendelea kufungamanisha utalii na utamaduni katika matamasha hayo.
“Naishukuru Kamati ya maandalizi
kwa kutafsiri vyema maono ya Rais Samia, katika sekta ya utalii kwani kupitia
tamasha hili tumeshuhudia shughuli mbalimbali zinazofanyika zikiwemo shughuli
za utamaduni na michezo, hivyo Wizara itaendelea kushirikiana na waratibu wa
matamasha haya ili kuwa karibu zaidi ili kuweza kufikia makundi yote hususani
watoto wadogo, ambao ndio lengo kuu la Wizara katika kuwarithisha utamaduni.”amesema.
Aidha amevisistiza vitengo vya idara
katika Wizara hiyo, kuhakikisha mazao ya matamasha haya yanabuniwa ili kuweza
kuwa vivutio vikubwa katika katika tasnia hiyo.
Katika Tamasha la Utalii Same
awamu ya pili, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dk. Pindi Chana, utoa tunzo
mbalimbali kwa wadau ili kutambua mchango wao katika kufanikisha tamasha hilo.








