KILEO-MWANGA.
Wakristo nchini wametakiwa kutafakari mahusiano yao na Mungu,
kisha kukabidhi maisha yao kwa Yesu Kristo aliyebeba amani ya kudumu ndani ya
maisha yao.
Akihubiri Desemba 22,2024 katika ibada ya kusimikwa kwa
mchungaji wa Kanisa la Africa Mission Evangelism Church Tanzania (AMEC),
Parokia ya Kileo, Wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro;
Katibu wa Theolojia Mchg. Yuda Kundael Pallangyo, Jimbo la
Arusha, amesema Wakristo, waliopata neema ya kusherehekea Sikukuu ya kuzaliwa
kwa Yesu Kristo, ni muhimu kujua kwamba Mungu, amejifunua katika maisha yao na
kwa kutafakari hilo, amewataka kukabidhi maisha yao kwa Yesu Kristo, aliyebeba
amani ya kudumu ikiwa na majibu ya changamoto zao.
Akinukuu maandiko katika Biblia takatifu, Mchg. Pallangyo,
amesema ujio wa Yesu Kristo, ulitabiriwa na manabii kabla ya kuzaliwa kwa
mwanadamu aliyefanya miujiza mikubwa, akauwawa kabla ya kufufuka na kupaa
mbinguni, baada ya maisha ya miaka 33 duniani, hivyo kifo chake ndio msingi wa
ahadi ya Mungu kuunganisha upya, mahusiano yake na mwanadamu kwa ajili ya
kumwagika damu.
Aidha Mchg. Huyo, amewasihi Wakristo hasa wale wanaopitia
changamoto na hali ngumu, kuwa na subri na imani na kuwasihi kutokukata tamaa
pindi wanapokuwa wakipitia changamoto mbalimbali za maisha.
Mchg. Pallangyo, amesema wakati wa Mungu unapofika huwainua watu
kutoka chini na kuwapa baraka na mafanikio, licha ya changamoto na hali ngumu
za maisha wanazozipitia kwani Mungu ana njia ya kuwainua na kuwapa neema wakati
wake.
Aidha amesema mbele ya uso wa Mungu hakuna kudhaurika na
kwamba mtu ambae anakuona ni wa chini, Mungu anakwenda kumwinua na kuwa mtu wa
viwango vingine huku akitolea mfano katika mji wa Nazareth ambao ulikuwa
unaonekana hauwezi kutoa mtu mashuhuri, lakini alikuja kutokea mtu ambaye ni
mwana wa Mungu nae ni Yesu Kristo.
“Wako baadhi ya watu wanasema inawezekanaje watu wa Parokia ya
Kileo wakapata mchungaji, wako watu wa Jimbo la Kilimanjaro watasema
inawezekanaje Kanisa la AMEC lenye waumini wachache kiasi hiki likatoa
mchungaji? Nataka nikwambie…Bwana ana mpango wa kuliinua kanisa lake na anapoliinua
kanisa lake analiinua kutoka katika eneo ambalo huwezi kutarajia, kama
ilivyokuwa kwenye mji wa Nazereth uliokuwa ukidhaurika lakini Masihi ndipo
alipotokea pale.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Furaha Tanzania, Jones
Mola, amewasihi waumini kuwajibika kwa wachungaji wao kwa kuwatembelea na
kuwatunza, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano na msaada wa viongozi wa
kiroho.
Askofu Mola aliweka wazi kwamba wachungaji ni vionyesho vya
huduma ya Mungu kwa watu, na ni jukumu la waumini kuwasaidia ili waweze
kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha Askofu Mola amewasihi wakristo waliojiunga na kanisa
la AMEC, wasikubali kurudi nyuma, kwani wako baadhi ya watu watakuja na
kuwalaghai kwamba kujiunga na kanisa hilo watakuwa wamepotea na hivyo
kukatishwa tamaa.
Katika ibada hiyo Askofu Mkuu wa Kanisa la Africa Mission Evangelism Church Tanzania (AMEC) Baltazari Kaaya, alimsimika Mchungaji Pauli Mark Assey, kuwa Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la AMEC Parokia ya Kileo.