MOSHI-KILIMANJARO
Wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri hapa
nchini, wametakiwa kuhakikisha kwamba wanakuwa mfano mzuri, katika kurejesha
fedha hizo kwa wakati ili watu wengine waweze kuendelea kukopa.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini Priscus Tarimo, ameyasema hayo, wakati akishuhudia
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu akikabidhi hundi ya mfano yenye thamani
ya Sh milioni 813.4 kwa vikundi vya 65 vya wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu.
Tarimo amewataka wale wote waliochukua mikopo hiyo kuirejesha kwa wakati
ili kutoa fursa kwa vikundi vingine viweze kukopeshwa.
Aidha amewataka wajasiriamali hao kuwa mabalozi wazuri kwa kuwahamasisha
watu wengine kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo hiyo.
“Fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa na halmashauri zinatokana na
ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri, hivyo amewasihi wafanyabishara
kuhakikisha wanalipa kodi za serikali kwa usahihi pasipo kukwepa.”amesema
Mbunge Tarimo.
Akizungumza
katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo iliyofanyika katika viunga vya Manispaa
ya Moshi mkoani humo, Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa hiyo Mwl. Mwajuma Nasombe, amesema
tangu Rais Samia Suluhu Hassan, akamate wadhifa huo manispaa ya moshi imekwisha
kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bil. 2.5 hadi kufikia mwaka 2023.
Mwl.
Nasombe amesema, baada ya kuwapatia mikopo hiyo, wakazi wa Manispaa ya Moshi waliokidhi
vigezo kwa mwaka huu, Wataalam wa Manispaa hiyo, wataanza kuwapatia elimu jinsi
ya kuendesha miradi, utunzaji wa fedha, ujazaji wa mikataba na utunzaji wa
kumbukumbu.
Hata hivyo Nansombe; amewataka waliokopeshwa kutorudia makosa ya
awali yaliyofanya wakati fulani mikopo hiyo kusitishwa kutokana na wengine
kushindwa kurudisha ambapo hadi sasa Manispaa hiyo inavidai vikundi kiasi cha Sh
milioni 956.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia halmashauri zake imekuwa ikitoa
mikopo ya asilimia 10 kwa wananchi wake kama sehemu ya juhudi za kukuza
maendeleo ya kiuchumi na kupunguza umaskini.














.jpg)