MOSHI-KILIMANJARO
Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi, imewaomba viongozi wa vyama
vya siasa mkoani Kilimanjaro, kuwahamasisha wanachama, wafuasi na
mashabiki wa vyama vyao, kujitokeza kwa
wingi katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo linatarajiwa kufanyika kwa siku saba
kuanzia Desemba 11 hadi 17 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Mtibora Seleman, ametoa wito
huo, wakati wa uwasilishaji wa mada kuhusu maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura, kwa wadau wa uchaguzi mkoani Kilimanjaro.
Katika uwasilishaji wa mada yake hiyo Seleman, amewaomba
viongozi wa vyama vya siasa kutumia majukwaa
na mitandao ya kijamii, kuwahamasisha wanachama wao kujitokeza kwa siku saba
zilizotolewa na (INEC), kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la uboreshaji wa
daftari la kudumu la wapiga kura.
Amesema zoezi la uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura
linawahusu wale wote ambao hajaandikishwa
katika daftari la wapiga kura na tayari wametimiza miaka 18 na wale
ambao watatimiza miaka 18 katika siku ya uchaguzi mkuu mwaka 2025 na wale ambao
wamepoteza kazi zao.
Aidha amesema kwenye mkoa wa Kilimanjaro Tume Huru ya Taifa
ya Uchaguzi inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 180,540, ikiwa ni ongezeko
la asilimia 18 ya wapiga kura 1,009726 waliopo kwenye daftari la kudumu la
wapiga kura.
“Jumla ya asasi za kiraria 157 zimepewa fursa ya kutoa elimu
ya mpiga kura katika zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura,” na
kuongeza kuwa utaratibu wa wafungwa, INEC imefanya maboresho katika uandikishaji
kwa kutoa fursa kwa wafungwa waliofungwa chini ya miezi sita na mahabusu ambao
hawajahukumiwa kuzshiriki katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapiga kura,”amesema.
Kwa upande wake Mjumbe
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Balozi Omar Ramadhan Mapuri, amewataka wadau
ambao wameshiriki katika mkutamno huo kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ambao
hawakupata nafasi ya kushiriki katika mkutano huo.
Mkutano wa Tume na Wadau wa Uchaguzi kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura, umewakutanisha wadau mbalimbali wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa, asasi za kirari, wahariri wa vyombo vya habari, watu wenye ulemavu, viongozi wa dini, vikosi vya usalama, vijana na viongozi wa kimila.














